Breaking News

Oct 6, 2020

SHIRIKA LA WORLD VISION TANZANIA YAWANUFAISHA WANANCHI KILOSA


Huduma bora zizolewazo na World vision ni pamoja kuwafanya wanafunzi wawe na nyuso za furaha na matumaini katika maisha yao ya baadae

Na Mwandishi wetu
SHIRIKA lisilo la Kiserikali,World vision Kanda ya kati limetumia zaidi ya mil.30 katika kuihudumia jamii katika maeneo ya vijijini yakiwemo,Mtumbatu na Magoleni Wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro katika kukamiliana na changamoto za upungufu wa madawati,bima ya afya kwa kaya maskini na ununuzi wa vyarahani 35 kwa vijana wahitaji.

Meneja wa World vision Kanda ya Kati,Faraja Ulanga alibainisha hayo katika risala yake kwa mgeni rasmi,Katibu tawala wa Wilaya ya Kilosa Yohana Kisitila kwenye hafla fupi ya utoaji wa taarifa ya shughuli za kijamii zinazotolewa na taasisi hiyo katika kuwasaidia jamii katika nyanja za elimu,afya na ujasiriamali kwa vijana waliomaliza darasa la saba lakini hakuweza kuendelea na elimu ya sekondari.

Ulanga alisema kuwa World vision ilipokea maombi kutoka kwa jamii kupitia ofisi yako ya Magole kuhusiana na mahitaji na changamoto zilizopo katika jamii,kwamba kuna vijana wanaomaliza darasa la saba lakini hawana ujuzi wala shughuli za ujasiriamali hivyo wanahitaji vyarahani kwa ajili ya kuendesha shughuli za uzalishaji zinakazowaongezea kipato ndani ya familia zao na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Mbali na hilo pia alisema taasisi yake imeweza kutengeneza madawati  madawati 100 kwa shule ya Msingi Mtumbatu, ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayosimamia sera ya elimu bila malipo kutoka shule ya awali hadi sekondari kidato cha nne.

Aidha alitaja eneo lingine ambalo taasisi hiyo imeshughulikia ni kuwakatia bima ya afya watoto wanaotoka katika familia yenye kipato kidogo ambapo jumla ya watoto 2910 ili waweze kupata huduma ya matibabu bila ya vikwazo,kwa kuwa sera ya world vision ni  pamoja na kumsaidia mwanajamii kuwa na afya njema.

"World vision tumeelekeza nguvu zetu kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali,ambapo leo tutawakabidhi vyarahani 35 kwa ajili ya kuwawezesha vijana  katika shughuli za ujasiriamali,watoto 2910 tumewatia bima ya afya,madawati 100 kwa shule ya msingi Mtumbatu vyote hivi vina thamani ya shilingi mil 31,475,000 " alisema.

Kwa upande wake Katibu tawala Wilaya ya Kilosa, Yohana Kisitila alishukuru shirika la World vision Tanzania,kanda ya kati kwa mchango wake katika jamii,kwamba serikali inatambua kazi nzuri zinazofanywa na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi hiyo hivyo atatoa wito kwa mashirika mengine kuendelea kuihudumia jamii.

Kisitila alisema kuwa hatua ya shirika la world vision  kwa kuwakatia bima ya afya kwa watoto 2910 wanaoshi katika mazingira magumu,vyarahani 35 kwa vijana na msaada wa madawati 100 kwa shule ya msingi Mtumbatu ni jambo lenye tija na msaada mkubwa kwa jamii katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo umaskini wa kipato.

 Neema Cyprian ni miongoni wa wanufaika na msaada wa vyarahani, akiongea kwa niaba ya wenzake alishukuru uongozi wa world vision kwa kuwajali na kuisaidia jamii hivyo na kwamba watatumia vema msaada wao kwa kuanzisha kikundi cha ushonaji wa nguo ili waweze kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kuwanufaisha wao wenyewe,familia na jamii inayowazunguka.

No comments:

Post a Comment