Breaking News

Sep 23, 2020

ZAO LA KUROSHO KUKABILI ATHARI ZA UKAME KONGWA


Mkuu wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma,Seleiman Serera aliyesimama akisisitiza umuhimu wa kilimo cha korosho  kwa maafisa ugani hawapo pichani 
Na Ashton Balaigwa,Kongwa

SERIKALI wilayani Kongwa,mkoani Dodoma imedhamilia kupunguza ukame na athari za mabadiliko ya tabia nchi na  kuifanya wilaya hiyo kuwa ya kijani kwa kupanda miti mingi ya zao la korosho ambayo pia itasaidia kukuza uchumi wa wanachi wilayani humo.

Kwa kuanzia tayari wilaya hiyo ya Kongwa imeshapanda miti ya mikorosho 306,886 ambayo sawa na ekari 10229.5 ambayo kwa kiasi kikubwa imeanza kupunguza tatizo la ukame linaloikabili wilaya hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Suleiman Serera wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kilimo cha korosho kwa maafisa ugani na wakulima wa zao hilo yanayotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele na kufanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa,ili kufikia malengo hayo tayari wameanzisha mkakati wa kila kaya inakuwa na ekari moja wa zao la korosho katika jumla ya kaya 74,000 zilizopo katika wilaya hiyo na tayari uhamasishaji umeshaanza kufanywa kwa watalaam wa kilimo na viongozi wa Serikali kupita nyumba hadi nyumba kutoa elimu.

“ Wilaya yetu inatatizo la ukame sasa tumekubalina na Wakala wa Misitu tupande miti mbalimbali ya mazao na matunda ikiwemo mikorosho na tayari imeshapandwa na tumeona mafanikio na ukame umeanza kupungua “ alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Kongwa.

Kwa upande wake Afisa Kilimo,Ushirika na Umwagiliaji,Jackos Shija,alisema kuwa tayari wameshaagiza miche 2,220,00 ya mikorosho kutoka TARI Naliendele  kwajili ya kuzipatia kaya hizo zianze kupanda zao hilo la korosho na kutokana na umuhimu wa zao la korosho linalosaidia kurejesha uoto hali ya  asili.

Shija alisema kuwa pamoja na zao hilo kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi lakini pia mkakati ni kulifanya zao hilo kuwa la kudumu na la kibiashara ambalo litaongeza kipato cha mkulima na kuifanya wilaya hiyo sasa kukua kiuchumi.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa  zao la korosho kutoka TARI Naliendele Dk Geradina Mzena,alisema mkakati uliopo wa Serikali ni kulifanya zao hilo la korosho hapa nchini kuzalishwa kwa wingi katika mikoa yenye fursa ikiwemo mkoa wa Dodoma na wilaya zake kwakuwa mahitaji ya korosho ni makubwa katika nchi za ulaya .

Dk Mzena alisema kuwa ili kufikia malengo hayo TARI Naliendele imeamua kuja na mikakati mipya ya kutoa elimu juu ya mbinu bora za kilimo cha korosho pamoja na matumizi ya viuatilifu na mbegu bora ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa zao la korosho hapa nchini.


No comments:

Post a Comment