Breaking News

Aug 30, 2026

MSIGWA: MAADILI NA UTAMADUNI VIKO HATARINI

 MAADILI NA UTAMADUNI VIKO HATARINI
 

Na Thadei Hafigwa

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, hali ambayo imeifanya serikali kutoa nafasi kubwa kwa viongozi wa kimila, wakiwemo Machifu, kushiriki katika juhudi za kusimamia na kuenzi maadili na utamaduni wa Mtanzania.

Msigwa, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema hayo Agosti 29, 2026, wakati akifunga Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika katika Viwanja vya Jamhuri mkoani Morogoro.

Tamasha hilo liliwakutanisha vikundi vya ngoma za asili kutoka mikoa mbalimbali nchini, sambamba na maonesho ya vyakula, mavazi na bidhaa nyingine za asili.

Alisema kasi ya utandawazi na maendeleo ya teknolojia imeleta changamoto katika uhifadhi wa utamaduni wa Tanzania, hivyo kuwepo kwa umuhimu wa jamii, viongozi wa kimila na vyombo vya habari kushirikiana kuhakikisha mila, desturi na maadili mema yanaendelea kuhifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Msigwa aliwataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao katika kukuza na kutangaza utamaduni wa Tanzania, akisisitiza kuwa utamaduni unaweza kuwa chanzo muhimu cha fursa za kiuchumi kwa wananchi.

“Leo hii nchini kwetu kijana mdogo kumtukana mtu mzima inaonekana ni kitu cha kawaida. Mimi ni baba na mtoto wangu wa kwanza ana umri wa miaka 25, lakini cha kusikitisha ni kwamba anashuhudia watoto wadogo wakinitukana mitandaoni,” alisema Msigwa.

Katika kuelezea changamoto za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Msigwa alisema hata yeye amewahi kukumbana na taarifa za uongo zilizosambazwa mitandaoni kuhusu familia yake.

Alisema wakati akiwa njiani kuelekea kwenye tamasha hilo alipokea jumbe nyingi za pole baada ya kusambaa kwa taarifa za uongo zilizodai kuwa mama yake amefariki dunia.

“Hata nilipokuwa nakuja hapa nilikuwa napokea pole nyingi kwa sababu kuna watu wameandika mitandaoni kuwa mama yangu amefariki. Nataka niwaambie kuwa mama yangu hajafa, ni mzima wa afya na yupo kijijini Iringa anaendelea na shughuli zake kama kawaida,” alisema.

Msigwa alisema moja ya dhamira ya serikali ni kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unarithiwa na vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa unafundisha misingi ya kuheshimiana, kusaidiana na kupendana.

“Maadili na malezi yanaanzia nyumbani, hivyo niwaombe Watanzania tuwe waangalifu na maudhui yanayotangazwa au kuchapishwa mitandaoni,” alisema.

Aidha, aliwataka wadau wa utamaduni kujenga mazingira yatakayowezesha bunifu mbalimbali kustawi na kutumika kama sehemu ya kukuza uchumi wa wananchi.

Kupitia tamasha hilo, Msigwa pia aliwakumbusha Watanzania kujielekeza katika kutafuta na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, hususan kuelekea matukio makubwa yatakayofanyika nchini, ikiwemo mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

No comments:

Post a Comment