Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Mhandisi Martine Ntemo akizungumza na wanamichezo, walimu, maafisa michezo na utamaduni wakati wa hafla ya kufunga michuano hiyo ya shule za msingi UMITASHUMTA ngazi ya Mkoa wa Pwani ambapo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wakuu wa idara.
WACHEZAJI 100 PWANI WAPENYA KWENYE CHEKECHE LA UMITASHUMTA
NA VICTOR MASANG, PWANI
JUMLA ya
wachezaji wapatao 100 wamechaguliwa kwa ajili ya kuweza kuunda
kikosi cha timu ya Mkoa wa Pwani ambacho kitashiriki katika kinyanga’nyoro
cha michezo mbalimbali kwenye kivumbi cha Mashindano ya umoja wa
michezo na taalumu kwa shule ya za msingi (UMITASHUMTA) ngazi ya Taifa ambayo
inatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake mwanzoni mwa mwezi huu Mkoani
Mtwara.
Hayo yamebainishwa na Afisa Michezo wa Mkoa wa Pwani Grace
Buleta wakati wa kufunga rasmi michuano ya UMITASHUMTA ngazi ya
Mkoa na kubainisha kuwa kabla ya kuchagua kikosi hicho cha wachezaji 100
kuliweza kufanyika mashindano katika michezo mbali mbali ambayo yaliweza
kuwajumuisha wanamichezo kutoka halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani na ndipo
jopo la kamati ya michezo kwa kushirikiana na maafisa michezo waliweza
kuwachagua wachezaji kwa kuzingatia vigezo.
Buleta aliongeza kuwa hapo awali wachezaji ambao walishiriki
katika mashindano ya ngazi ya Mkoa kwa ajili ya kupata kikosi hicho walikuwa
zaidi ya 650 lakini kwa sasa baada ya michuano hiyo kumalizika waliweza
kuwachagua baadhi ya wachezaji ambao wana vipaji na uwezo kwa lengo la kuweza
kuunda kikosi cha Mkoa kilichokuwa bora.
“Tunashukuru hii hatua ya mwanzo tumeweza kuikamilisha ya kupata
wachezaji 100 ambao wataunda timu ya Mkoa wa Pwani na kwamba sio kwamba wengine
hawana uwezo lakini tumehakikisha kwamba tunawachagua wale wachazaji ambao
wameweza kuonyesha uwezo wao katika kipindi chote za mashindano hayo na nia
yetu kubwa ni kufanya vizuri katika mashindano ya Taifa,”alisema Buleta.
Aidha Buleta alifafanua kuwa kwa sasa mipango ambayo wameiweka
ni kuiweka timu ya Mkoa kambini kwanza kwa muda nne hadi kwa ajili ya
kuweza kuwapa fursa walimu na makocha waweze kutoa maelekezo mbali mbali
ambayo yatawasaidia wachezaji kujifunza mambo mbali mbali ikiwemo sheria na
taratibu ambazo zitakwenda kutumika katika mashindano ya Taifa.
“Zoezi la kuchagua kikosi cha timu ya Mkoa wa Pwani kwa upande
wetu tumelifanya kwa kuzingatia usawa katika kila pande na kwamba katika
michuano hii tumeweza kuwachagua wachezaji katika michezo mbali mbali ikiwemo
mpira wa miguu, mpira wa mikono, netiboli, Riadha, mpira wa wavu, pamoja na
fani mbali mbali za ndani ikiwemo ngoma na kwaya,”alifafanua Buleta.
Katika hatua nyingine Buleta aliongeza kwamba katika michuano ya
msimu wa mwaka huu wa 2021 wamejipanga vizuri hivyo wanatarajia kuipeperusha
vema bendera ya Mkoa wa Pwani na kurudi na ubingwa na kuwaomba wadau, mashirika
na umma na taasisi binafsi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa sapoti ya
hali na mali kwa kikosi hicho kilichoundwa cha Mkoa wa Pwani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha injinia Martine Ntemo
ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mashindano hayo kwa niaba ya Mkuu wa
Mkoa wa Pwani amewataka wanamichezo hao kuhakikisha kwamba wanajitadi kwa
uwezo wao wote kufanya vizuri katika mashindano hayo ya Taifa kwa lengo
la kuweza kuibuka na ubingwa na kurudi na vikombe ili kuutangaza vema Mkoa wa
Pwani katika Nyanja ya michezo.
Pia Ntemo aliwasisitizia kwamba wanamichezo ho hao kuhakikisha
wanachukua tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa mbali mbali na kuziagiza
halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya viwanja vya michezo kwa
wanafunzi hao sambamba na kuwanunulia sare za michezo na kuwataka pia wanafunzi
hao kuwa na nidhani katika kipindi chote na michuano hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la elimu Kibaha Robert Shilingi
akitoa salamu zake alisema kuwa wachezaji wote ambao wamechagulia kunda kikosi
cha timu ya Mkoa kupambana vilivyo na kutumia fursa hiyo katika kuonyesha
vipaji uwezo walionao katika michuano hiyo ya ngazi ya taifa ili kurudi na
ubingwa ambao utaweza kuwa na tija zaidi katika sekta ya michezo ndani ya Mkoa
wa Pwani.
No comments:
Post a Comment