MBUNGE WA JIMBO LA KIBAHA MJINI(KATIKATI MWENYE SUTI NYEUSI),SILVESTRY KOKA AKIKABIDHI MFANO WA HUNDI KWA WAWAKILISHI WA VIKUNDI VYA VIJANA,WANAWAKE NA WALEMAVU KWA AJILI YA MKOPO USIYO NA RIBA ULIOTOLEWA NA HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA KUTOKA MAKUSANYO YAKE YA NDANI
HALMASHAURI
ya mjini Kibaha iliyopo mkoani Pwani imetoa kiasi cha
shilingi milioni 312 kwa ajili kuviwezesha vikundi vya vijana,wanawake na walemavu ikiwa ni kutekeleza
maagizo ya serikali ya kutenga asilimia 10 katika makusanyo ya ndani kwa
ajili ya kuwapatia mikopo ambayo haina riba kwa makundi
hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kibaha George Mbogo
alibainisha kuwa kwa kipindi cha mwaka 2020 /2021 kupitia idara ya
maendeleo ya jamii imeweza kuhamasisha wananchi kuunda vikundi vya kijamii
ambapo jumla ya vikundi 327 kutoka katika kata 14 viliweza kuundwa na kusajiliwa.
Kaimu mkurugenzi huyo alifafanua kuwa Halmashauri ya mji KIbaha
imeweza kujenga kituo cha biashara kwa wanawake wajasiriamali kilichopo kwenye
soko la mnarani pamoja na eneo maalumu la kuuzia kuku kwa madhumuni ya kuinua
zaidi biashara zao kwa kuanzisha mitandao yao.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Selina Wilson
alibainisha kwamba pamoja na mafanikio hayo lakini bado kuna changamoto
ya ucheleweshaji wa kurejesha mikopo hiyo hasa katika baadhi ya makundi ya
vijana na kuwataka kuhakikisha kwamba wanarejesha kwa wakati bila kuvunja
taratibu zote zilizowekwa ili kuwapa fursa wengine waweze kupata.
Selina aliongeza kuwa mbali na halmashauri hiyo kutoa mikopo ya
fedha, pamoja na vifaa mbalimbali lakini wanatarajia kuongeza wigo zaidi ya
ukopeshaji ambao wameweka mikakati kabambe katika siku za usoni kuwezo
kuvipatia vikundi mbali mbali mikopo mikubwa zaidi ikiwemo kuwapatia magari
ambayo yatawasaidia katika kuendeshea biashara zao
Akikabidhi hundi ya fedha hizo ambazo zimetolewa na halmashauri
hiyo kwa vikundi hivyo,Mbunge wa jimbo la Kibaha
mjini Silvestry Koka ambaye alikuwa ndiye mgeni rasmi
katika hafla hiyo iliambatana na ugawaji wa vifaa vinavyofanya shughuli za
usafirishaji ikiwemo Bajaji, Pikipiki.pamoja na Toyo vyote vikiwa na thamani ya
zaidi ya milioni 66 ikiwa ni kujikwamua kiuchumi.
Koka katika hotuba yake kwa wanavikundi hao aliwataka kuhakikisha
kwamba fedha hizo ambazo wamepatiwa na serikali kuzitumia vizuri kwa
kufanya shughuli za ujasiriamali pamoja na kuanzisha biashara ambazo
zitawasaidia kujipatia kipato ikiwemo na kukuza uchumi.
Pia Mbunge huyo aliviasa vikundi hivyo kujiwekea malengo na
kwamba ili waweze kutimiza ndoto zao na kufanikiwa inapaswa waahakikishe kwamba
wanakuwa na nidhamu katika fedha sambamba na kubuni biashara nyingine mpya ambazo
zitaweza kuzaa matunda na kuwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha.
Aidha, alisema kwamba wananchi pamoja na viongozi wa ngazi
mbali mbali kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele katika kumpa ushirikiano
wa kutosha Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan ili aweze kutumiza
majukumu yake ipasavyo katika kulitumikia Taifa la Tanzania pamoja na kuwaletea
chachu ya maendeleo wananchi katika Nyanja mbalimbali.
Koka alisema kwamba anatambua katika jimbo lake kuna baadhi ya
changamoto zilizopo hasa za miundombinu ya barabara inayokwenda katika
hospitali ya Wilaya iliyopo maeno ya Lulanzi na kuwaahidi wananchi wake
kulivalia njuga suala hilo kwa kushirikiana na serikali na mamlaka husika ili
kuweka kiwango cha lami ili iweze kupitika kwa urahisi na wananchi waweze
kwenda kupatiwa huduma ya matibabu bila kero yoyote.
No comments:
Post a Comment