Breaking News

Jun 24, 2021

DC WA BAGAMOYO ANZA KAZI,AKUTANA NA WAKUU WA IDARA CHALINZE NA BAGAMOYO

Mkuu wa Wilaya mpya ya Bagamoyo, Zainabu Issa (wa katikati) akizungumza na wakuu wa Idara mbalimbali kutoka Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze,kulia kwake ni Katibu Tawala wa Wilaya  Bagamoyo, Kasilda Mgeni na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi.

DC WA BAGAMOYO ANZA KAZI,AKUTANA NA WAKUU WA IDARA CHALINZE NA BAGAMOYO

NA VICTOR MASANGU,CHALINZE

MKUU mpya wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Issa amewataka watumishi na wakuu wa idara wote kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia weledi,nidhamu na kutenda haki bila ya kumwonea mtu yoyote kwa kuzingatia misingi ya Sheria na taratibu.

Kauli hiyo, ameitoa wakati alipofanya ziara yake ya kwanza ya kikazi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na kuamua kuwakutanisha wakuu wote wa idara mbalimbali kutoka halmashauri za Bagamoyo pamoja na Chalinze kwa lengo la kujadili mipango ya kimaendeleo na changamoto zilizopo.

Mkuu huyo, ambaye aliongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Bagamoyo amesema kwamba anamshukuru Sana Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu kumuamini na kumteua kuwa mkuu wa wilaya hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

''Mimi lengo langu kubwa na kikao hiki ni kukutana na wakuu wa idara ambao nina imani kubwa ndio wataweza kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku lakini kitu kikubwa ni lazima kuwe na nidhamu katika suala zima la uwajibikaji ikiwemo pamoja na kutenda haki kwa kila mmoja,"alisema mkuu huyo.

Pia, alibainisha kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kwamba inawasaidia wananchi kutatua changamoto na kero zao ambazo zinawakabili katika sekta mbalimbali ikiwemo  afya,maji miundonbinu ya barabara,elimu pamoja na Mambo mengine ya msingi.

Aidha, mkuu huyo, kupitia kikao hicho aliwakumbusha wakuu hao wa idara kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kwamba wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa fedha ili kutimiza malengo waliyojiwekea.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa Wilaya, aliwataka watumishi hao kuhakikisha kwamba waachana kabisa na tabia ya kukaa maofisini na badala yake wabadilike kwa kuwatembelea wananchi ili kubaini changamoto zinazowakabili. 

Kadhalika, alisema atahakikisha kwamba anashirikiana bega kwa bega na watumishi wote wa halmashauri za Chalinze pamoja na Bagamoyo na kuwataka wawe kitu kimoja na kupeana ushauri katika mambo mbalimbali.ikiwemo kuwaletea wananchi maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni amemhakikishia mkuu huyo  mpya wa wilaya kumpa ushirikiano na mshikamano wa hali ya juu na kwamba nia ya serikali ya awamu ya sita ni kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo, Fatma Latu wamempongeza mkuu huyo kwa uamuzi wa kuwakutanisha wakuu wa idara ambao wataweza kuwa kitu kimoja na kuyatekeleza maagizo yote yaliyotolewa.

No comments:

Post a Comment