Breaking News

May 20, 2021

WAZIRI MKUU AKEMEA WANAOWANYANYASA WAANDISHI WA HABARI

WAZIRI MKUU AKEMEA WANAOWANYANYASA WAANDISHI WA HABARI

Na Ashton Balaigwa,MOROGORO

WAZIRI Mkuu,Majaliwa Kassim Majaliwa,Ameonya Viongozi wa Serikali wamekemea tabia ya baadhi ya watu wanaowanyanyasa Waandishi wa habari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao,kuacha tabia hiyo  na wale watakaendelea kufanya hivyo Serikali haitawavumilia na badala yake  itawachukulia hatua kali.

Alisema sio sera ya Serikali ya kuwaonea waandishi wa habari na kwamba haitamvumlia kiongozi au mtu yoyote atakayemkwaza Mwandishi wa habari akiwa katika kazi ya Uandishi wa habari na kuhakikishia waandishi wa habari kuchukua hatua kali na itaendelea kuimarisha misingi ya habari hapa nchini.

Waziri Mkuu alitoa onyo hilo,wakati akifungua Mkutano mkuu wa Jukwaa la  Wahariri wa mwaka (TEF) na Kongamano la Kitaaluma (Editors Retreat) wa siku tatu ambao utaenda sambamba na uchaguzi wa viongozi watakaongoza katika kipindi cha miaka minne unaofanyika mjini Morogoro.

Alisema kuwa serikali inawatambua na kuwathamini waandishi wa habari kutokana na kazi yao kubwa wanayofanya ikiwemo ya kuchochea shughuli za maendeleo zinazotekezwa na serikali hivyo isingependa kuona hata siku moja mwandishi anapata tatizo pale anapotimiza wajibu wake .

“ Mchango wenu waandishi wa habari ni mkubwa mno na serikali inautambua kwakuwa mmekuwa mkisaidia kuchochea katika shughuli za maendeleo hivyo kama serikali tusingependa kuona kuna mtu anawaonea wakati wa kutimiza wajibu wenu” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa,alisema,Tanzania ni moja ya nchi katika Afrika ambazo zinaongoza kuwa na vyombo vingi vya habari ikiwemo Magazeti,Radio,Television na TV Mtandaoni na hiyo inatokana na kutambua mchango mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari kutokana na mshikamano uliopo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

“Waandishi wa habari ni watu muhimu sana na sisi kama serikali tutaendelea kuwatumia na kuwatumia huku kunatokana na thamani ya mchango mnaotoa na tutahakikisha mnalindwa pale mnapokuwa katika kutekeleza majukumu yake ya aundishi wa habari” alisema.

Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa  alisema pamoja na ushirikiano uliopo lakini aliwataka waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria,kanuni,weledi na kutanguliza uzalendo wa Taifa lao kwakuwa hawana nchi nyingine isipokuwa Tanzania.

Akizungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari,aliwataka waandishi kuzingatia sheria za nchi,wasitumie vibaya kalamu zao kwani kalamu hizo ni muhimu sana na isimuonee mtu na itumike katika kusimamia haki ya kila mmoja na serikali kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM) imeweka bayana mpnago wa kuboresha mazingira ya wanahabari nchini na kuhakikisha uhuru wa kupata habari na uhuru wa kutoa habari unaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa sheria.

Akijibu hoja ya Kaimu Mwenyekiti wa TEF ,Deodatus Balile,kuhusu madeni ya serikali yanayodaiwa na vyombo vya habari na kusababisha hali mbaya ya kiuchumi kwenye vyombo hivyo,Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza vyombo vya serikali,wizara na taasisi zinazodaiwa ifikapo june 30 mwaka huu ziwe zimeshalipa madeni yake.

Aliagiza Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo kuweka mpango na mkakati wa kushirikisha vyombo vya habari kikamilifu na kuharakisha mchakato wa kuundwa bodi ya Hithibati itakayofanya kazi ya kusimamia maadili ya taaluma ya habari na kuwezesha kuwa na baraza huru la habari.

Awali,Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Innocent Bashungwa,alisema tayari kuna maazimio yaliyotolewa kwenye siku ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na kama wizara wapo tayari kuyapitia na kufanya maboresho sehemu zenye changamoto kwa waandishi wa habari.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa TEF,Balile,aliomba viongozi wa kitaifa kama Rais,Makamu na Waziri Mkuu kuwa na utaratibu wa kukutana na wahariri na waandishi wa habari kwa ajili ya kujadililiana kuhusu maendeleo ya nchi kwa manufaa ya watanzania.

Kaimu mwenyekiti huyo alisema kukutana huko kutaweza kusaidia kuchochea maendeleo ya wananchi kutokana na vipaumbele vinavyoelekezwa na serikali.

 

No comments:

Post a Comment