Munira Hussein
Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine barani Afrika, ni nadra kwa wanawake kugombea ama kutia nia kwa nafasi za juu za uongozi katika nchi zao.
Hivi sasa mchakato wa kuchukua fomu za uteuzi wa kugombea nafasi za urais wa nchi hiyo kwa kipindi cha mwaka 2020-2025 unaendelea.
Vyama mbalimbali vya kisiasa kupitia wawakilishi wake ambao ni wagombea wa nafasi za urais tayari wamechukua fomu za uteuzi wa Urais.
Hadi sasa wagombea zaidi ya vyama 10 vya kisiasa wamechukua fomu hizo, wagombea wanawake hawakua nyuma kutia nia zao katika nafasi kubwa zaidi nchini humo.
Queen Cathbert Sendinga kutoka chama cha alliance for democratic change (ADC) alichukua fomu ya kutia nia mwishoni mwa juma lilipita akitaka kuidhinishwa kwa upande wa Tanzania bara.
Bi sendinga anaamini kuwa wanawake wakikabidhiwa madaraka hufanya vizuri.
''Wanawake wengi ambao wanapewa madaraka huwa wanafanya vizuri na mimi nimeona kuwa sasa ni wakati muafaka kuingia na kuwa kiongozi wa kuleta maendeleo nchini Tanzania'' anasema Bi Sendinga.
''Hatua ya urais inahitaji mtu ambae ni muelewa, muadilifu, asiyekua na makundi na mchapaji kazi, na mimi sifa zote hizo ninazo, na pia mi ni mama, na mama ni kiongozi kutoka ngazi ya familia'' ameongeza Bi Sendinga.
Amesisitiza pia juu ya nia yake ya kukomboa Tanzania hususani Watanzania wa hali ya chini Kiuchumi.
''Ukuaji wa uchumi wa mtu unatakiwa kwenda sawa na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, sawa maendeleo yamefanyika lakini lakini je mtanzania mwenyewe anaishi vipi? Anawezaje kujikimu na Maisha yake ya kila siku?.''
Mgombea mwingine aliyechukua fomu za uteuzi kutoka tume ya taifa ya uchaguzi ni Bi Cecilia Augustiono Mwanga.
Bi Mwanga amechukua fomu za uteuzi wa urais kama muwakilishi wa chama chake cha Demokrasia makini.
Bi Mwanga ameahidi kuwa kama atapitishwa kuwa mgombea na tume ya taifa ya uchaguzi, basi atasimamia suala la kilimo na pia atafanya kampeni zake kwa kutumia usafiri unaotumika sana vijijini, kama Baiskeli na Guta.
''Nataka kuwadhihirishia Umma watakapo nichagua mimi, nitahikikisha nawasimamia watu wa hali chini, wakulima, hatutawabagua tunataka kunyanyuka nao, na tumejipanga na chama chetu. Anasema bi Mwanga.
Mchakato kwa wagombea hawa
Wagombea hawa pamoja na wagombea wengine wa urais kutoka vyama mbalimbali nchini Tanzania, wanaendelea na zoezi la kuchukua fomu za uteuzi kutoka tume ya taifa ya uchaguzi.
Wanahitajika wawe wamerudisha fomu hizo hadi kufikia tarehe 25 ya mwezi Agosti, kisha Tume ya uchaguzi ya nchi ikijiridhisha basi watapitishwa na kuwa wagombea rasmi wa Urais na makamu Rais wa Tanzania.
"Itakapofika siku ya Uteuzi tarehe 25 Agosti, 2020 mtarejesha fomu zenu hapa Tume, na Tume baada ya kujiridhisha kuwa mnazo sifa itawateua"alisema Jaji Kaijage. Anasema Jaji Semistocles Kaijage mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Tanzania (NEC)
Wagombea wanawake wana nafasi kiasi gani?
Kwa mujibu wa utafiti wa uliofanywa na taasisi ya wanawake ya umoja wa matifa (UN women) mwaka 2019, umeonesha kuwa baadhi ya vyama vya siasa vimekua vikiwakwamisha wanawake kutokana na mfumo dume ya vyama hivyo.
Lakini kama ilivyo kwa wagombea wengine, wanawake pia wanahitajika kuwa na sera na ushawishi wa kutosha ndani ya vyama vyao na kwa jamii kwa ujumla.
Katika uchaguzi wa mwaka 2015, mgombea pekee mwanamke kutoka chama cha ACT wazaelendo Anna Mghwira hakufanya vizuri katika uchaguzi huo, lakini alipata sifa kemkem kutoka pande nyingi, na baadae akateuliwa na Rais John Magufuli kuongoza mkoa wa kaskazini mwa Tanzania.
Lakini pia kwa mara ya kwanza Tanzania imefanikiwa kuwa na makamu wa kwanza wa Rais ambaye ni mwanamke, mara baada ya kuchaguliwa kama mgombea mwenza wa Rais wa sasa wa Tanzania John Magufuli mwaka 2015 katika mchakato wa ndani wa chama cha mapinduzi CCM.
Wanawake wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kisiasa nchini Tanzania lakini pia changamoto nyingi zinawakabili.
Mafanikio ya wanawake kisiasa barani Afrika
Siku za hivi karibuni wanawake barani Afrika wamekua wakishiriki katika masuala ya uongozi na siasa idadi kubwa zaidi.
Mbali na kuwa na wanawake wachache walipitia nafasi za Urais barani Afrika, baadhi ya nchi zimeanza kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye siasa na masuala ya uongozi.
Katika baadhi ya nchi, wanawake wamekua wakiongoza mihimili mbalimbali kama Bunge.
Katika nchi za Gambia, Madagascar, Malawi, Mozambique, Rwanda, South Africa, Togo, Uganda, Mabunge yao yaongozwa na spika wa wanawake.
Kwa upande wa nchi ya Rwanda zaidi ya asilimia 60 ya bunge lake lina wawakilishi wanawake, ikiwa ni nchi yenye mafanikio zaidi kuwa na uwakilishi wa hali ya juu wa wanawake katika nyadhifa za uongozi.
No comments:
Post a Comment