Breaking News

Sep 25, 2024

BRELA YAWAHUDUMU WANANCHI USAJILI WA KAMPUNI KWENYE MASHINDANO SHIMIWI MOROGORO


Na Thadei Hafigwa,Morgoro

KATIKA hali ya kuwaletea huduma wanachi kwa karibu,Wakala wa usajili wa Kampuni na leseni wameonesha ubunifu wa kipekee katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara,Taasisi na Idara za Serikali yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Morogoro kwa kuweka banda la kutolea huduma kwa wananchi.

Akiongea na waandishi wa Habari Mjini Morogoro,muda mfupi baada ya ufunguzi wa mashindano ya Shimiwi,Robert Mashika Afisa Leseni wa Brela amesema kuwa BRELA imeshiriki katika mashindano hayo kwa mwaka huu imeleta timu ya mpira wa miguu na Netboli ikiwa ni kutimiza maelekezo ya serikali na kuhamasisha afya za watumishi katika maeneo ya kazi.

Mashika amesema kuwa mbali na hayo wametumia fursa hiyo ya mkusanyiko wa wadau wa michezo na wananchi wanaofika katika uwanja wa Jamhuri kushuhudia mashindano hayo kwa kuweka banda la kutolea huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi hiyo.

“BRELA kama wakala wa usajili wa biashara na Leseni inatoa huduma ya usajili wa kampuni,Majina ya biashara,usajili wa hataza,usajili wa alama za biashara na huduma pamoja na utoaji wa leseni za biashara kundi A,pamoja na leseni za viwanda.”alisema

Aidha,alisema kuwa wamepata mwitikio mkubwa wa watu kwa ajili ya kufanya sajili  na kurasimisha biashara zao, pamoja na kupata elimu Brela.Alitoa  wito kwa wakazi  wa Morogoro na viunga vyake,sanjari na wadau wote walioshiriki katika mashindano hayo kufika katika banda hilo ili waweze kuhudumiwa.

Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara,Taasisi na Idara za Serikali kwa mwaka 2024 ni 38 ambayo yameshirikisha vilabu 57,yamefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Doto Mashaka Buteko akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.

Miongoni mwa waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adam Kighoma Malima,Naibu Waziri wa Sanaa,Utamaduni na Michezo,Hamis Mwinjuma,Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Musa Kilakala na Meya wa Manispaa ya Morogoro,Paschal Kihanga.

Kabla ya Mashindano hayo kufunguliwa,wanamichezo waliingia kwa maandamano wakiwa wameshika mabando yenye ujumbe mbalimbali ikiwemo kuhamasisha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment