WIZARA YA ELIMU KUKABIILI UFAULU MDOGO SOMO LA HISABATI
Na Lilian Lucas, Morogoro
Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imeanza kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ufaulu mdogo wa
somo la Hisabati kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwa kuanzisha
mafunzo maalumu kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa
Wakufunzi wa somo hilo wa Vyuo 35 vya Ualimu nchi nzima ili kuongeza kiwango
cha ufaulu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa Carolyne Nombo, amesema hayo leo Julai
11,2923 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kazini kwa wakufunzi 155 wa somo la
Hisabati kutoka Vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali yanayoendelea mjini Morogoro.
Profesa Nombo amesema
mafunzo kwa wakufunzi hao ni moja ya utekelezaji wa lengo la serikali katika
kuleta mageuzi katika somo la Hisabati.
Profesa Nombo amesema mpango
huo wa Serikali utaimarisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la
hisabati ikiwa pamoja na kutumia TEHAMA katika kipindi ambacho Serikali inatekeleza
mageuzi ya elimu nchini.
Amesema katika kufanikisha
mpango huo wa kuinua ufaulu wa somo la hisabati,tayari Serikali kupitia wizara
hiyo ya Elimu imewekeza kwenye ujenzi wa majengo mapya na kuimarisha
miundombinu ikiwemo maabara na kuanzisha majengo mapya ya TEHAMA kwa kila chuo
cha ualimu.
“Sisi sote tunafahamu kuwa kuna changamoto ya ufaulu katika somo la hisabati, mazingira ya kufundishia si mazuri hivyo serikali yetu imeamua kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika vyuo vya Ualimu ili viweze kutoa walimu tarajali watakaofundisha somo hilo kwa shule za Msingi na Sekondari” amesema Katibu Mkuu huyo.
Baadhi ya wakufunzi 155 wa somo la Hisabati kutoka Vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali wakisfuatilia kwa makini katika mafunzo ya uboreshaji wa somo la Hisabati mjini Morogoro.Picha na.Lilian Lucas.Profesa Nombo amesema tayari Serikali imewekeza kwa kujenga kituo cha Hisabati katika Chuo cha Ualimu Morogoro na kimewezeshwa vifaa mbalimbali vya kisasa vya kitehama ikiwemo Vishkwambi, Kompyuta ambavyo kwa pamoja vinawezesha wakufunzi hao kujifunza hata wakiwa nje ya vituo vyao.
“Wakufunzi wote
watapitishwa kwenye matumizi ya mifumo ya somo la hisabati ,matumizi ya
vishikwambi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia na kuwajengea mbinu za
kufundisha hisabati kwa kutumia TEHAMA”amesema.
Amesema baada ya mafunzo
hayo wakufunzi hao watakwenda kuwawezesha walimu tarajali ambao nao watakwenda
kufundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuinua ufaulu wa somo hilo la hisabati.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Mafunzo ya Ualimu ,Huruma Mageni, amesema Wizara ya Elimu inaendelea na
utekelezaji wa kazi mbalimbali za mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu (TESP)
ikiwemo kutoa mafunzo kazini kwa wakufunzi
wanaofundisha somo la hisabati.
Mageni amesema mafunzo hayo
yanatolewa kwa wakufunzi wanaofundisha mafunzo ya ualimu wa ngazi ya Cheti na
Diploma kutoka katika vyuo hivyo vyote 35 vya Ualimu vya serikali ambayo yanatolewa
kwa njia ya mtandano.
Mratibu wa Mradi wa
Kuendeleza Elimu ya Ualimu, Cosmas Mahenge amesema mafunzo hayo ya Hisabati kwa njia ya TEHAMA yanatolewa kwa
wakufunzi kutoka kanda ya kaskazini, mashariki, nyanda za juu kusini, kanda ya
ziwa, magharibi, kati na kusini kwa lengo la uboreshaji wa somo hilo.
Mshauri mwelekezi wa mradi
huo wa TESP, Dk Andrew Binde amesema wameanza na wakufunzi wa somo la Hisabati
kwa kuwa tayari miundombinu yake imekamilika kwenye vyuo vya Ualimu kutokana na
kuanzishwa kwa vituo vya TEHAMA na baadae kuinua katika masomo mengine.
Kwa upande wake, mkufunzi
wa somo la Hisabati, Gloriana Kakuru kutoka Chuo cha Ualimu Morogoro amesema
mafunzo hayo yatawasaidia kuwatia moyo hasa wanawake kuwa somo sio gumu na
wajiamini kuwa wanaweza ili kufanya vyema katika masomo ya Hisabati na Sayansi.
Aidha, mkufunzi kutoka Chuo
cha Ualimu Kleruu cha mkoani Iringa Kissa Mboya amesema mafunzo hayo yatakuwa
msaada kwao kama wakufunzi wanaowandaa walimu na kutarahisisha kuandaa masomo
na nyaraka za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo njia ya mawasiliano kwa kutumia
majukwaa mbalimbali ya Hisabati.
No comments:
Post a Comment