Breaking News

Jul 6, 2023

TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI

          Mkurugenzi mtendaji wa Global Water Partnership Tanzania, Dk Victor Kongo

BAADA YA WANANCHI KUSHIRIKISHWA:

TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI

Na Lilian.Lucas,Morogoro.

TAASISI ya kimataifa ya Global Water Partnership kwa kushirikiana na Wizara ya Maji imefanikiwa kupunguza suala la uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kuwashirikisha wananchi kwenye maeneo yao.

Aidha, mkurugenzi wa huduma za kisheria kutoka Wizara ya Maji Simon Nkanyemka, amesema Tanzania imeonyesha kufanya vyema katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi baada ya wananchi kushirikishwa kikamilifu kwenye miradi ya kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji inayopekwa kwenye maeneo yao.

Amesema hayo, mjini Morogoro wakati wa warsha ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi wa rasilimali za maji iliyowashirikisha wataalamu kutoka  Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu na wataalamu wa maji kutoka nchi ya Botswana.

Nkanyemka amesema katika kustahimili mabadiliko hayo ya tabia nchi, taasisi ya kimataifa isiyo ya kiserikali ya Global Water Partnership kupitia mradi wa pamoja unayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwashirikisha wananchi na wataalamu kwani kwa kufanya hivyo itasaidia vyanzo vya maji kubaki salama.

Amesema kwa upande wa Tanzania, mradi huo wa mabadiliko ya tabia nchi umetekelezwa katika bonde la Wami Ruvu Morogoro ikiwa ni pamoja na kujenga Vinywesheo vya mifugo kwa ajili ya kusaidia wafugaji kutopelekea mifugo kwenye mito.

“Hiyo kwa kiasi kikubwa imesaidia na kuweza kupunguza shughuli za kibinadamu katika mto Ruvu ambao umekuwa ukitegemewa kwa ajili ya usambazaji maji kwa jiji la Dar es salaam na kwa kuchukua hatua hizo imepunguza kukauka kwa mto,”amesema.

Washiriki wa warsha ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi wa rasilimali za maji kutoka  Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu na wataalamu wa maji kutoka nchi ya Botswana.Picha na Lilian Lucas.

Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Elibarik Mmassy amesema kwa miaka mitatu wamekuwa wakishirikiana na taasisi ya Global hasa kwenye maeneo ya usimamizi na utunzaji vyanzo vya maji na kwamba pamoja na kupitia changamoto mbalimbali za upatikanaji wa maji lakini taasisi hiyo imekuwa bega kwa bega kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa kwa kubadilishana uwezo.

Mmassy amesema, katika kipindi cha kuanzia 2022 na 2023 wameanza kushirikiana kwenye ujenzi wa Birika la kunyweshea mifugo lenye uwezo wa kunywesha mifugo 4,000 kwa siku, kuchimba kisima cha mita 120, na kujenga tanki lenye mfumo wa sola ambapo mradi huo umekamilika.

Amesema “Mto Ruvu unategemea sana safu za milima ya Uluguru na kwa eneo la usimamizi hatukuwa na ofisi kwa eneo la Mvuha na sasa ofisi iko mbioni kukamilika na itawezesha kusogeza huduma kwa wananchi hasa katika ngazi ya kijiji na mito zaidi ya sita itatiririsha maji na imekuwa ikitachangia asilimia themanini(80) ya maji kwenye mto Ruvu.”

Naye, Mkurugenzi mtendaji wa Global Water Partnership Tanzania, Dk Victor Kongo amesema nchi ya Botswana na Tanzania zilichaguliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa mabadiliko ya tabia nchi, kwamba Wami Ruvu ni bonde linalokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Dk Kongo amesema mradi wa mabadiliko ya tabianchi upo chini ya ufadhili wa Umoja wa nchi za Ulaya (European Union) kupitia Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC),ambapo maeneo yaliyoelekezwa na kuhitaji kusaidiwa ni Ruvu darajani yenye mifugo mingi wakati wa kiangazi ukimbilia ndani ya mto kunywa maji na ufanya uhalibifu wa kingo.

Alisema hali hiyo imepelekea wafugaji wameingia kwenye  sintofahamu kutokana na  kero wanayopata baada ya mifugo yao kukamtwa wakati wakiingiza mifugo kwenye mito na vyanzo vya maji,huku baadhi ya akina mama upata shida ya mamba waliopo mwenye mito.

No comments:

Post a Comment