Sehemu ya Mto Duthumi uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambapo kina chanke kimepungua kutokana na shughuli za kibinadamu
Na Thadei Hafigwa
MISITU ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinayotegemewa
katika maisha ya binadamu na viumbe hai vingine ambayo inayopaswa kuhifadhiwa
na kulindwa.
Misitu ni mkusanyiko
wa miti ya asili au iliyopandwa na binadamu katika eneo kubwa la
kijiografia.Zipo faida nyingi zinatokanazo na misitu ikiwemo vyanzo vya maji.
Misitu ina faida
kubwa katika maisha yetu ya kila siku,karibu kila siku tunatumia bidhaa za
misitu.Uhifadhi misitu na ulinzi wa
vyanzo vya maji ilikuwa ni sifa ya Milima ya Uluguru iliopo Mkoani Morogoro.
Hali ni tofauti sasa. Shughuli za kibinadamu
ikiwemo kilimo,ukataji miti kwa ajili nishati ya mkaa na kuni
kumechangia kupoteza sifa hiyo. Kadhalika, mifugo
kuingia kwenye misitu ya hifadhi ambako kuna vyanzo vya maji kumeongeza
uharibifu wa mazingira.
Mkoa wa Morogoro una mito 143.
Baadhi ya mito hiyo ikiwemo Mvuha na Duthumi huungana na Mto Ruvu ambao maji
yake yanahudumia wakazi wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Baadhi ya mito hiyo ipo kwenye misitu ya hifadhi na mingine inasimamiwa na Halmashauri
ya vijiji,lakini majira ya kiangazi maji ya mito hiyo hupungua kina chake na mingine
hukauka,ambapo. mwaka 2022 wananchi wa mikoa ya
mitatu ya Pwani,Morogoro na Dar es Salaam walikabiliwa na uhaba wa maji kwa
kupata maji kwa mgao.
Ripoti ya Mwezi Agosti 2022
iliyotolewa na Mamlaka ya Bonde ya
Wami Ruvu inaeleza kuwa wastani wa kina cha maji katika kituo cha Ruvu
kilichopo Mkoa wa Pwani karibu na mtambo wa DAWASA wa Ruvu juu ilikuwa 1.68m.
Kiwango hicho kwa mujibu wa Mamlaka
ya Bonde la Wami Ruvu, hakitoshelezi mahitaji kwa upande wa kidakio cha Ruvu
ambapo mtiririko wake unakadiriwa kuwa na lita 19,730 kwa sekunde.
Katika kipindi hicho, baadhi ya
watu wenye visima binafsi vya maji wa mikoa hiyo inakuwa ni neema kwao kwa
kuuza maji. Ujazo wa lita 20 huuzwa kwa shilingi kati ya 500 hadi 1,000 na
kusababisha wananchi walio wengi kutumia gharama kubwa kupata huduma hiyo ya
maji.
Athari hiyo haikuishia kwa
watumiaji wa maji majumbani pekee bali pia wenye viwanda ambapo uzalishaji wa
bidhaa hupungua kutokana na mashine za kufua umeme wa nguvu ya maji kufanya
kazi kwa kiwango cha chini.
Maeneo mengine mifugo ilikufa kwa kukosa malisho na maji.
Elizabeth Mnyamili (50) ni mkazi wa
Kijiji cha Visakazi,kutoka jamii ya wafugaji Chalinze,Mkoa wa Pwani. Anasema kipindi cha kiangazi ambacho ni
kuanzia Agosti hadi Novemba walikabiliwa na ukosefu wa malisho na maji kwa
mifugo yao na kusababisha mifugo kufa.
“Mwaka 2022 kutokana na ukame
mifugo ilimekosa malisho na maji,
ng’ombe wangu 50 wamekufa kwa njaa,”alisema Elizabeth Mnyamili mkazi wa Chalinze
Pwani.
Taasisi ya Utafiti wa Misitu
Tanzania (TAFORI) ni miongoni mwa taasisi zilizofanya ufafiti juu ya athari za
uharibifu wa mazingira na kubaini ya kuwa shughuli za binadamu zimechangia
kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira na kuathiri vyanzo vya maji
vinapatikana kwenye misitu.
Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya
Misitu Tanzania (TAFORI),Dkt.Revocatus Musumbusi alisema kuwa kwenye misitu
ndiko kwenye vyanzo vingi vya maji ambapo takwimu zinaonesha kuwa uharibifu wa
misitu hapa nchini ni kiasi cha hekta 469,420 kwa mwaka.
Dkt.Musumbusi alibainisha kwamba
chanzo kikuu cha uharibifu huo ni pamoja na uvamizi katika baadhi ya maeneo ya
hifadhi za misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo,malisho ya mifugo,uchimbaji
wa madini,makazi na ukataji haramu wa miti kwa ajili ya nishati (mkaa),mbao na
nguzo za ujenzi.
“Kiasi cha misitu iliopo nchini Tanzania ni hekta milioni 48
ambapo uharibifu wa mazingira kwa mwaka ni hekta 469,420. Uharibifu huo unatokana na kuwepo kwa shughuli za binadamu
ikiwemo kilimo cha kuhamahama,”alisema
Dkt.Musumbusi.
Alisema kuwa, kilimo kinaathiri
mazingira kwa kiwango kikubwa. Watu
wanafika kwenye misitu,wanakata miti,wanachoma moto,wanalima wakifikiri kwamba
maeneo hayo yana rutuba,na kwamba wanapomaliza kulima mwaka mmoja,mwaka
unaofuata wanahamia katika eneo lingine na kuchangia uharibifu wa misitu.
Eneo lingine alilobainisha, ni
malisho ya mifugo,kwamba mifugo inapoingia msituni kwa lengo la kutafuta
majani, inakanyaga miti michanga na mimea mingine.
Pessa Mohamed Pessa Mkazi wa
Duthumi anasema uharibifu wa mazingira kwenye misitu ya Kijiji ni mkubwa
kutokana na kuwepo kwa wimbi la wageni walioingia kiholela eneo hilo na kujitwalia
ardhi bila ya utaratibu.
Pessa alisema kuwa, baadhi ya
viongozi wa vijiji wanakosa uweledi katika usimamiaji wa sheria na ulinzi wa
mazingira na vyanzo vya maji licha ya
kuwepo kwa sheria zilizopitishwa na Bunge.
Sheria ya Mazingira No.5 ya Mwaka
2004 ambayo imeanza kutumika Julai 1, 2005 ni nyezo muhimu ya kulinda na
kusimamia shughuli zote za mazingira.sheria
inaamuru uwepo wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji katika kusimamia kikamilifu mazingira kwenye eneo
husika.
Chesco Nagileki (44) ni kiongozi
wa wafugaji mkazi wa Duthumi katika wilaya ya Morogoro vijijini anaeleza
changamoto walionayo wafugaji ni kutokuwa na malambo ya kunyweshea mifugo maji
kwamba wanalazimika kupeleka mifugo maeneo yenye mito.
Nagileki anakiri kuwa mara kadhaa
wafugaji wanalalamikiwa kupeleka mifugo kwenye vyanzo vya maji,na kutafuta
malisho ya mifugo kwenye misitu.
Alisema mwaka 2009 kijiji chao
kiliweka mpango wa matumizi bora ya ardhi. Wafugaji walitengewa ekari 4592 kwa
ajili ya kuendesha shughuli za mifugo lakini wafugaji bado hawajaruhusiwa
kulitumia eneo hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbwade
Morogoro vijijini,Salumu Maloso anasema nyakati za kiangazi Kijiji chake
kinakabiliwa na changamoto ya jamii ya wafugaji wanachunga mifugo yao kiholela
kwa kutafuta malisho kwenye misitu na kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji.
Maloso anasema kuwa ofisi ya
Kijiji inatumia kamati ya mazingira ya Kijiji katika kushughulikia changamoto
za wafugaji kuingia mifugo kwenye vyanzo vya maji lakini wakati mwingine
inafanyakazi chini ya kiwango kwa sababu wajumbe wanakuwa na majukumu mengine
ya kiuchumi kwenye familia zao.
“Kamati ya mazingira iliyopo
kwenye Kijiji changu inafanya kazi kutegemeana na matukio, lakini pia
wanawaelimisha wafugaji kudhibiti mifugo yao lakini matukio yamekuwa
yakijirudiarudia mara kwa mara,”alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Morogoro, Lucas Jaji Lemomo amekiri uwepo wa uharibifu wa mazingira
katika maeneo ya misitu na kwenye vyanzo vya maji,kwamba mkakati uliopo katika
halmashauri hiyo ni kupanda miti ili kunusuru misitu na vyanzo vya maji.
Msitu
ya asili Duthumi,Morogoro vijijini ilivyoathiriwa na shughuli za kilimo .(Picha
na Thadei Hafigwa)
“Tunashirikiana na wataalamu
kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) katika kuhakikisha misitu inalindwa ili
kufuatilia maeneo yote yalioharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu”alisema
Lemomo.
Lemomo anasema msitu wa Pangawe
ambao upo chini ya uangalizi wa Halmashauri ya Wilaya umeathiriwa na shughuli
za binadamu. Uharibifu wa mazingira ni mkubwa,lakini wapo katika mchakato wa
kuwaomba wataalamu kufanya utafiti kujua ukubwa wa uharibifu wa mazingira.
Alisema kuwa wakati wakiendelea
na mchakato wa kuwasiliana na wataalamu wa misitu kujua ukubwa wa uharibifu wa
mazingira kwa sasa halmashauri wanaendesha shughuli ya upandaji wa miti katika
maeneo yaliothiriwa na uharibifu wa mazingira ili kurudisha sifa ya Morogoro
katika utunzaji wa mazingira kama ilivyokuwa hapo awali.
“Changamoto ya wafugaji kuingia
kwenye vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira kwa kukosa majosho na malambo
Halmashauri imeshaanza mkakati maalum kwa kukabiliana na hali hiyo. Mchakato wa
ujenzi wa mabwawa mawili pamoja na majosho ya mifugo umeshaanza”
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kirutheri Dayosisi ya Morogoro,Jacob Mameo anahusisha kanisa kuwa ni taasisi
inayohudumia mwanadamu kimwili na kiroho,kwamba uhai wa mwanadamu
hautenganishwi na mazingira ambayo hayawezi kutenganishwa na huduma ya maji.
Askofu Mameo anasema kuwa ongezeko
la watu na mahitaji ya kiuchumi yanachangia uharibifu wa mazingira na kwenye
vyanzo vya maji na kusababisha kuwepo kwa athari hasi za kimazingira,ikiwemo
vyanzo vya maji kukauka.
Anasema kuwa, matukio ya uharibifu
wa mazingira maeneo ya vijijini ni mengi yanatishia uhai wa binadamu uvunaji wa
miti ovyo ni sawa na kuangamiza taifa. Iwapo ulegevu katika usimamizi wa sheria
ukiendelea katika matumizi ya rasiliamali za misitu ni sawa na kujiua wenyewe.
”Jamii ipapaswa kushiriki kupanda
miti,kulinda vyanzo vya maji na watu waloipewa dhamana ya kusimamia sheria
kutimiza wajibu wao bila ya upendeleo”alisema Askofu Mameo.
Juma Msike ambaye ni Kiongozi wa
mila ,Mkazi wa Tegetero, maarufu kwa jina la
Chifu Magoma wa Tegetero, Morogoro vijijini, anasema matukio ya
uharibifu wa mazingira yamekuwa yakijitokeza kutokana na kulegalega kwa
ushirikiano kati ya viongozi wa mila na serikali.
Chifu Magoma anasema kuwa kiongozi
wa mila anawaelekeza jamii anayoingoza kutoa taarifa kwa serikali ya kijiji pindi
wanapowatilia mashaka watu wanaoingia kwenye misitu ili kunusuru misituhi.
Alisema kuwa, hali hiyo miaka 20
iliyopita ilisaidia kuiweka misitu kuwa salama,lakini hali ya sasa ni tofauti.
Wageni wanapewa vibali na serikali za kuvuna miti na kusababisha matukio ya
uharibifu wa mazingira.kwa hiyo viongozi wa serikali wangewashirikisha viongozi
wa mila katika mchakato wa utoaji wa vibali kungesaidia kunusuru misitu.
“Nikiwa kiongozi wa mila nina
wajibu wa kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira,kuacha kukata miti ovyo. Jamii
inapaswa kutambua umuhimu wa kutunza misitu kwa kuwa tunaitumia kwenye shughuli
za kimila ikiwemo tambiko,”alisema.
“Watu wanaopewa vibali vya
uvunaji wa miti wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu kwa sababu ni chanzo cha
uharibu wa mazingira. Kwa kuvuna miti ovyo.msitu unaonekana kwa nje ipo salama lakini
ukiingia msituni imeharibiwz”.
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ni
taasisi yenye dhamana ulinzi na utoaji wa leseni ya uvunaji wa miti.Katika kuteleleza
majukumu yake inasimamia sheria ya Mazingira na.5 ya mwaka 2004,Sheria 4 ya Ardhi ya Mwaka 1999
pamoja na Sheria ya 5 Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999.
Sheria hizi zinawekwa kwa
vijiji kumiliki na kusimamia rasilimali za misitu katika ardhi ya kijiji na
kuzitumia katika misingi endelevu kwa kutengeneza na kusimamia sheria ndogo
kupitia amati za Maliasili na mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu.
Patricia Manonga ni Mhifadhi Misitu Wilaya ya
Morogoro,kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). Anasema kuwa jukumu alilokuwa
nalo ni kushirikiana na viongozi wa serikali ya vijiji ili kunusuru misitu na
vyanzo vya maji.
Manonga anasema misitu ya hifadhi
iliopo eneo lake la utawala ni Mvuha Chamanyani,Kimboza,Mkongwe,Ruvu na Mkulazi. Lakini pia
misitu ianatokao kwarikali za vijijini
zinazomiliki kwa kuhifadhi misitu anatoa ushauri wa kitaalamu kwa
kuzingatia sheria zilizopo.
No comments:
Post a Comment