Na Lilian Lucas,Dar es Salaam
WADAU wa sekta ya habari nchini wameshiriki katika Kongamano la
Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 Jijini Dar Es Salaam katika ukumbi wa
kimataifa wa Julius Nyerere international convention center(JNICC) ikiwa ni
mkakati wa serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliyojipambanua kuboresha demokrasia na uhuru wa kujieleza.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ambapo pamoja na kufanya ufunguzi alitoa tuzo kwa baadhi ya waandishi wa habari waliotoa mchango wao
katika kuhabarisha umma katika sekta ya madini,elimu na ujenzi.
Mada mbalimbali zilitolewa huku Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za waandishi wa Habari,Kenneth Simbaya alielezea mchango wa waandishi wa habari waliopo mikoani ukiwa mkubwa licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,Kenneth Simbaya alitoa mada mchango wa Klabu za waandishi wa habari katika Tasnia ya habari nchiniSimbaya alisema kuwa UTPC kwa kushirikiana na washirika wake
waliweza kufanikisha kuendesha midahalo mbalimbali ikiwemo uhuru wa kujieleza,haki
ya kupata taarifa na usalama wa waandishi wa habari.
“Tuliweza kuendesha midahalo na jeshi la Polisi mikoani,ombi letu
ni kuungwa mkono na serikali na wadau wengine katika kuhakikisha waandishi wa
habari wanafanya kazi kwa usalama”Alisema Simbaya.
Aliishukuru serikali ya awamu ya sita kuwa kuonesha utayari wake
katika kuhakikisha ya kuwa haki ya kupata taarifa inakuwa kipaumbele katika
kuimarisha demokrasia na utawala bora.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa TBC Dkt.Ayoub Lioba alielezea
mafanikio ya vyombo vya habari toka uhuru wa Tanganyika (Tanzania bara) mwaka 1961
kwamba kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika tasnia ya habari.
Dkt.Lioba alisema changamoto iliyopo katika sekta ya habari kwamba uwepo wa uhuru wa kupata habari uende sambamba na nini cha kufanya baada ya kuwa na uhuru wa habari.
Alisema kuwa badala viongozi wa kitaifa kufanya ziara kwenye
maeneo mbalimbali hapa nchini na kuibua ubadhirifu jukumu hilo linapaswa
kufanywa na waandishi wa habari kwa kufuata misingi ya habari za uchunguzi.
Hili ni kongamano la kwanza lililoandaliwa katika sekta ya habari
na kuwashirikisha wadau wa sekta ya habari kutoka maeneo mbalimbali nchini limefungua
ukurasa mwingine wa kujadili na kutoa mapendekezo ya kuboresha sekta ya habari
hapa nchini.
No comments:
Post a Comment