Breaking News

Nov 3, 2022

ULINZI WA MISITU VIJIJI KUONGEZWA KUDHIBITI UCHOMAJI WA MOTO


ULINZI WA MISITU VIJIJI KUONGEZWA  KUDHIBITI UCHOMAJI WA MOTO

Na Lilian Lucas, Morogoro.

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imewataka wenyeviti na kamati za Maliasili na Mazingira za vijiji vyenye misitu ya asili kuongeza juhudi katika Ulinzi wa Misitu kwenye maeneo yao kwa kuimarisha doria za mara kwa mara kwa faida yao wenyewe na Serikali.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Ally Makoa aliyasema haya wakati akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa kijiji cha Chabima kata ya Masanse Wilaya ya Kilosa mara baada ya kutembelea Msitu wa kijiji hicho unaohifadhiwa kupitia Mradi wa Mkaa Endelevu unaosimamiwa na Shirika la uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) pamoja na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA).

Makoa alisema pamoja na kuwepo kwa kamati ya ulinzi na kijiji kupata manufaa mbalimbali ya msitu wajitahidi kujitahidi kuendelea kutunza misitu.

“Tumetembea huko kwenye msitu tumeona uchomaji wa moto msituni na umeonekana kukithiri kwenye maeneo mengi ya Kilosa pamoja na kuwepo kwa maeneo yaliyohifadhiwa ambayo yanaleta manufaa kwa kijiji husika, halmashauri na taifa letu bado juhudi zaidi zinahitajika kuhukuliwa katika uhifadhi,”alisema.

Aidha, Mwenyekiti hiyo alisema kuwepo kwa Msitu kunapatikana hewa safi, mvua, mazao ya misitu kama mbao, mkaa na kwamba watahakikisha wanafanya ushawishi wa mradi huo kuendelea kuwepo kwa manufaa ya wananchi.

Meneja wa Mradi kutoka TFCG, Charles Leonard alieleza kuwa uhifadhi na utunzaji wa misitu iliyopo kwenye Ardhi ya vijiji hapa nchini endapo rasilimali misitu itaendelea kuhifadhiwa vyema itapelekea misitu hiyo kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wanavijiji na taifa.

Leonard alisema kuwa faida zinazopatikana kwenye misitu hiyo ya vijiji ni pamoja ikolojia na kuimiri mabadiliko ya tabia nchi,na kwamba kiwango cha upotevu wa misitu nchini ni hekta 460,000 kwa mwaka jambo ambalo ni hatari.

Alisema “Huo upotevu unatokana na uhalibifu na upoteevu wa misitu hivyo tunatakiwa kuangalia namna ya usimamizi madhubuti wa misitu ili kupunguza kiwango hicho cha upotevu huo na jenzo ya usimamizi shirikishi ya jamii inawea kuwa jenzo ya kimkakatia katika kuokoa maeneo ya misitu yanayopotea nchini katika ngazi za vijiji,”.

Kwa mujibu wa ripoti ya Nafoma ya mwaka 2015 Tanzania inakadiriwa kuwa eneo la misitu hekta 48.1 milioni ambayo ni asilimia 55 ya eneo la ardhi nchini, idadi kubwa ya misitu hiyo ipo kwenye ardhi za vijiji ambayo ni asilimia 47, na asilimia 33 ipo kwenye ardhi iliyohifadhiwa ya Serikali inayosimamiwa na wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS).

“Eneo kubwa la misitu ipo ardhi za vijiji ambayo inagubikwa sana na uharibifu,misitu iliyotengwa na kusimamiwa na vijiji ni hekta 2 milioni kati ya hekta 22 milioni ambayo ni asilimia 47 ya misitu yote tu,hivyo zaidi ya hekta 19 milioni hazijatengwa na kuhifadhiwa rasmi,”alisema.

Afisa Maliasili Mkoa wa Morogoro Joseph Chuwa alisema kuwa asilimia 50 ya misitu yote nchini ipo kwenye Serikali za vijiji na asilimia 50 iko Serikali kuu kwa maana ya misitu inayonayolindwa kisheria kama hifadhi za taifa, na maeneo mengine.

Chuwa alisema kuwa, mpango ambao umeonyeshwa na Tfcg kupitia mradi huo wa mkaa endelevu na usimamizi shirikishi na manufaa yanayopatikana ndio pekeee inayoweza kutumika kuokoa misitu nchini.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Chabima Marygoreth Mrengeli alisema kuwepo kwa mradi huo kumenufaisha na kuwezesha kijiji kuwa na ofisi ya kijiji,Zahanati, kujenga vyumba vya madarasa, kuwepo kwa mradi wa mbao, mkaa endelevu.

Mrengeli alitaja fedha zilizopatikana kwa kipindi cha miaka minne kuwa ni 2018 -2019 sh 8.66 milioni, 2019 -2020 sh 21.81 milioni,2020 -2021 sh 59.34 milioni, mwaka 2021 – 2022 zilizopatikana ni sh 55.4 milioni na mwaka wa fedha 2022 – 2023 sh 430,000.

Mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi, kulinda, na kuwanufausha wakazi wa vijiji na kwa wilaya ya Kilosa Vijiji 20 vinanufaika na mradi huo.

No comments:

Post a Comment