Breaking News

Oct 26, 2022

VIJANA 150 WENYE ULEMAVU WA AKILI WAPATA ELIMU YA UJASILIAMALI


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la MWAYODE,Venance Mlali

VIJANA 150 WENYE ULEMAVU WA AKILI WAPATA ELIMU YA UJASILIAMALI

Na.Lilian Lucas,Morogoro

WAKATI Serikali inafanya jitihada ya kuhakikissha vijana nchini wanakuwa na uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa, shirika lisilo la kiserikali la Mafinga Women And Youth Develoment Organization (MWAYODEO) limeunga mkono juhudi hizo kwa kuwawezesha Vijana 150 wenye ulemavu wa akili Manispaa ya Morogoro kwa kuwapa Elimu ya stadi za kazi, ufundi wa aina mbalimbali ili waweze kuanzisha shughuli za ujasiliamali.

Elimu hiyo itawanufaisha kwa kuwaletea maendeleo yao binafsi, wazazi na walezi wao kutokana na kipato watakachokipata baada ya kununuliwa kwa bidhaa wanazozalisha.

Mkurugenzi mtendaji wa Mwayodeo,Venance Mlali alisema hayo  mjini Morogoro katika mkutano wa wadau wa Afya na Elimu ya Ufundi kwa Watu Wenye Ulamavu wa akili.

Mlali alisema Vijana hao wenye ulemavu wamenufaika na elimu hiyo (mafunzo) kutokana na utekelezaji wa Shirika kwa kushirikiana na Shirika la Vaasa Association for Developing Countries (VADCA) kutoka nchni Finland linalotekeleza mradi wa Fursa sawa za kupata stadi za ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili Tanzania (PROYOUTH).

Alisema kuwa vijana hao wamepatiwa mafunzio kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ( Veta Kihonda) na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Bigwa.

Aidha, alisema kuwa mradi umewajengea uwezo walimu wa vyuo vya ufundi 16 ambao wameshiriki kuwafundisha vijana wenye ulemavu wa akili  pamoja na uhamasishaji jamii kuhusu haki za vijana wenye ulemavu wa akili kushiriki kwenye mafunzo ya stadi za kazi na ufundi.

Alisema kuwa kupitia mradi huu vijana 150 wamepatiwa mafunzo katika fani ya useremala, Cherehani, ufugaji wa kuku, upishi, utengenezaji wa matofali  na uandaji wa miti na bustani.

Mlali alisema kutekelezwa kwa mpango huo kulitokana na utafiti uliofanywa na MWAYODEO na kubaini idadi hiyo ya vijana katika Manispaa ya Morogoro kuwa wana ulemavu wa akili na kusababisha shirika hilo kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwawezesha kupata elimu za stadi za maisha

“Kundi hili la vijana wenye ulemavu wa akili wanauwezo katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kujiingizia kipato chao hivyo ni lazima wawezeshwe ama kusaidiwa kwa namna moja ama nyingine,”alisema Mlali

“Kwa sasa Vyuo vya Ufundi vimetambua umuhimu wa kutekeleza Elimu shirikishi hususani kwa vijana wenye ulamavu wa akili ili kuwa waweze kukwamuliwa,” alisema Mlali

Alitaja changamoto zinazojitokeza ni uelewa mdogo wa familia zenye vijana wenye ulemavu huo na kusababisha ushiriki mdogo wa wazazi na walezi, vitendea kazi wanapomaliza mafunzo ili wajiendeleza zaidi na kuingiza kipato na baadhi yao kutependa kujiunga kwenye vikundi vya vijana ili vijulikane na halmashauri.

Nao baadhi ya wadau akiwemo mwalimu wa watu wenye ulemavu, Lilian Ngira alisema jamii inawajibu  wa kuacha kuwanyanyapaa kwani wengi wao wana uwezo wa kufanya kazi wanazofundishwa na kuelekezwa.

“Uelewa wao unachukua muda mrefu, jamii inatakiwa kuwaelewa na sio kuwanyanyapaa kama inavyofanywa kwa sasa,”alisema Ngira

Mmoja wa wazazi wa mtoto mwenye ulemavu  huo, Siasa  Omary alisema kijana wake alijifunza kwa muda wa miezi mitatu ufundi wa kushona na baada ya hapo uwezo wake ulikuwa mkubwa, awali changamoto aliyokuwa nayo ni usahaulifu vitu na kuogopa, lakini kwa sasa amepata kazi katika kiwanda cha ushonaji wa Jezi cha Mazava kilichopo mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment