SUA, WIOMSA YAWAKUTANISHA WANASAYANSI NA WADAU WA MAZINGIRA KUFANYA TATHIMINI UKANDA BAHARI YA HINDI
Na Lilian Lucas,Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kwa ushirikiano na Taasisi inayojishughulisha na tafiti za
utunzaji wa Bahari (WIOMSA) imewakutanisha wanasayansi, Mameneja na wadau
wengine wa mazingira ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuendesha na kufanya
tathimini ya maji kwa mazingira katika ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Akizungumza jana katika
mkutano wa mazingira wa kimataifa ambao wanapata mafunzo na kuwajengea
uwezo wadau hao wa mazingira Mkuu wa
Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune alisema baada ya kupata mafunzo hayo
watahakikisha wanakwenda kuyafanyia kazi na kuwafundisha wengine kwenye ofisi wanazotoka
ili kutimiza malengo.
Mfune alisema wale ambao
wako ukanda wa juu ya mto unakoanzia wanatakiwa kujua fika shughuli za
uharibifu wanazozifanya kule ndizo zinazopelekea athari kwenye mabwawa ambayo
hujaa tope na kwenda mojakwa moja Baharini na kuathiri viumbe vilivyomo katika
Mito, Maziwa na Bahari.
Mfune amewapongeza SUA na
WIOMSA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa yanaendana na kazi inayoendelea ya kurejesha
afya ya Mito na kupunguza madhara yanayotokana na uchafuzi wa Mazingira katika
mito, kwani ni jambo jema kufanyika na litakuwa msaada kwa Taifa.
Aidha amesema zipo shughuli
nyingi za kibinadamu zinazofanywa kwenye vyanzo vya maji na kandokando ya mito
nchini kama vile ukataji miti hovyo, ufugaji usionzingatia ukubwa wa eneo
ambapo amewataka Wananchi kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali
katika kusimamia sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhifadhi mito na mazingira
kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Maji yana umuhimu kwa
taifa zima kama bwawa la Nyerere ambalo linajengwa kwa gharama kubwa, iwapo
litashindwa kufanya kazi kutokana na ukosefu wa maji maana yake serikali
itakuwa imepoteza fedha hizo bure, lakini pia tuna bwawa la umeme la Mtera na
Kidatu haya yote yasipoweza kufanya kazi tutakuwa tunapunguza uwezo wa kuwa na
Tanzania ya viwanda,”alisema Mfaune.
Alisema wadau wengine wanatakiwa kuendelea kujitokeza kusadia jitihada za Serikali na wadau waliopo sasa ili kuhakikisha Mito inaendelea kutiririka maji kwa mwaka mzima na kwamba wananchi kutakuwa kuheshimu Sheria zilizowekwa kwa kuwa zipo kwa manufaa ya watanzania wote.
Akizungumzia mafunzo hayo
Mtafiti Mkuu wa Mradi kutoka (SUA) Profesa Japhet Kashaigili alisema lengo la
mafunzo hayo ni kujenga Wataalamu utaalamu wa kuweza kufanya tathimini ya maji
kwa mazingira ili kusaidia wanapofanya maamuzi katika kugawana maji iwe kwa
ajili ya maendeleo endelevu na si vinginevyo.
Profesa Kashaigili alisema mafunzo hayo yamelenga kujenga uwezo kwa vitendo na kuona shughuli zinazofanyika kama sehemu ya kuhifadhi mazingira na kilichopelekea shughuli hizo zifanyike pamoja sababu za msingi za kuwezesha tathimini ya maji kwa mazingira.
No comments:
Post a Comment