Breaking News

Oct 3, 2021

SERIKALI YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUFANYAKAZI KWA UWELEDI

Msemaji Mkuu wa Serikali ,Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wa Morogoro (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya Serikali. 

SERIKALI YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUFANYAKAZI KWA UWELEDI

Na Thadei Hafigwa

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka waandishi wa habari nchini kufanyakazi kwa uweledi kwa kuandika na kuibua habari zitakazosaidia kusukuma maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara za vijijini,madarasa na vituo vya afya ili nafasi ya vyombo vya habari katika kusukuma maendeleo iweze kupimika

Msemaji Mkuu wa Serikali Msigwa alibainisha hayo Mkoani Morogoro katika ukumbi wa mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa,wakati ikitoa taarifa ya wiki oktoba 2,mwaka huu juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kutoa taarifa hiyo kwa watanzania kila wiki.

 Msigwa alisema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuisaidia serikali katika kuripoti matukio na changamoto zinazowakabili wananchi hususan maeneo ya vijijini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi ambapo ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa waandishi wa habari watakaoibua taarifa zitakazoleta matokeo chanja ikiwemo ujenzi wa zahanati,kituo cha afya na ujenzi wa barabara na miundombinu.

Akizungumzia mwitikio kwa wananchi wa Morogoro katika kuchanja dhidi ya covid 19 imekuwa si ya kuridhisha hivyo amewataka wananchi kujitokeza ili kupata chanjo hiyo katika kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Kuhusu ujenzi wa barabara amesema serikali ipo katika hatua za awali za kujenga barabara ya kutoka Morogoro kuelekea Dodoma yenye urefu wa kilometa 267 kuwa itakapokuwa tayari barabara ya njia nne ili kurahisisha usafiri na usafirishaji katika njia hiyo.

Msigwa amesema kwa sasa Serikali anamtafuta Mkandarasi mshauri ili kuanza hatua za awali za Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo kwa ajili ya kuipanua ili kuwa na njia Nne yaani njia mbili kwa kila upande.

Akifafanua zaidi, Gerson Msigwa amesema malengo ya Serikali katika kupanua barabara hiyo, kwanza barabara hiyo ndiyo inayounganisha maeneo ya katikati ya nchi, lakini pia inaunganisha mikoa ya kanda ya ziwa na ukanda wa magharibi mwa nchi yetu, aidha amesema ndiyo kiunganishi kikuuu cha nchi ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Kongo na kwamba ni muhimu barabara hiyo ikaongezewa uwezo kwa kuwa inatumika kusafirisha mizigo inayokwenda katika nchi hizo jirani.

Katika hatua nyingine, Msemaji huyo wa Serikali amezungumzia ujenzi wa barabara ya  Mikumi - Kidatu – Ifakara yenye urefu wa Km 66.9 kutoka Kidatu – Ifakara, pamoja na ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu kwa kiwango cha lami.

Baadhi ya  waandishi wa habari  Mkoa wa morogoro  wakiwa katika picha ya pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali. kulia kwa Msemaji ni Mwenyekiti wa MOROPC,Nickson Mkilanya .

Amesema, barabara ya Kidatu–Ifakara ni sehemu ya barabara kuu itakayounganisha, Mikumi–Kidatu- Ifakara- Mahenge/Lupiro–Malinyi–Kilosa kwa Mpepo–Londo–Lumecha yenye urefu wa kilometa 547 ambayo inaunganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma kwamba barabara hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwa watanzania wakulima na wafanyabiashara wa mazao wa ukanda huo.

Katika kuhakikisha ya kuwa serikali ya awamu ya sita inatatua changamoto katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kusuasusa kwa ujenzi wa barabara ya Mikumi-Kidato hadi Ifakara kwamba usimamizi wa barabara hiyo umewekwa chini ya wakala wa barabara TANROAD ambapo viashiria vya mabadiliko hayo chanja yameanza kujidhihirisha mwezi septemba mwaka huu ambapo ujenzi barabara hiyo umefikia asilimia 37.5 ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment