Na Victor Masangu,Bagamoyo
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kwamba mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa daraja kubwa la mto wami unatarajiwa kukamilika novemba mwaka 2022.
Waziri huyo pia amemuagiza Mkandarasi anayejenga daraja hilo katika mto Wami kuhakikisha anaongeza Kasi kwa kuweka mipango ya kufanya kazi saa 24 ili kukamilisha kazi ya ujenzi huo kwa wakati.
Profesa Mbarawa, ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara yake ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi daraja hilo ambalo kutakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wasafiri na wafanyabiashara.
Aidha, aliongea kwamba ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake ulianza Oktoba 2018 matatarajio ilikuwa kukamilika mwezi Septemba 2021 lakini limechelewa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa mvua na ugonjwa wa UVIKO 19
Alimsisitiza Mkandarasi Kujenga daraja hilo kwa ubora unaotakiwa ili lidumu kwa muda mrefu na kuhakikisha ifikapo Novemba 2022 ujenzi uwe umekamilika.
Waziri Mbarawa, alisema daraja la awali lenye urefu wa mita 88.75 lilijengwa mwaka 1959 na kwa sasa lina uwezo mdogo wa kupitisha magari yanayoenda mikoa ya kaskazini na nchi za jirani kutokana na ongezeko la magari.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa barabara Mkoa wa Pwani (TANROADS) Mhandisi Andrea Kasamwa, alisema daraja hilo hadi kukamilika litagharimu Shilingi bilioni 72.
Mhandisi Kasamwa, amesema kuwa daraja hilo jipya litakuwa na urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 linajengwa umbali wa mita 670 pembeni ya daraja la zamani
Alisema tayari Mkandarasi amewasilisha sababu za kimkataba nyongeza ya muda wa Ujenzi kufika mwezi Novemba 2022.
Alisema kazi hiyo ya ujenzi inasimamiwa na makampuni mawili ya Ilshin ya Korea na Advanced Engineering Solution ya Tanzania.
Kasamwa aliongeza kuwa maendeleo ya
mradi huo hadi hadi kufikia Sasa tayari yamekamilika kwa kiasi cha asilimia
61.4.
No comments:
Post a Comment