Pori la Akiba Mpanga Kipengere kuongeza watalii 100,000 Kwa mwaka
Na Lilian Lucas, Njombe
MAMLAKA ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambao ni wasimamizi wa Pori la Akiba la Mpanga-Kipengere lililopo Wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe imetenga kiasi cha sh 1.57 bilioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi hiyo ya maendeleo ikiwemo kuboresha utalii na kufanya watalii kuongezeka kutoka 7,000 hadi kufikia zaidi ya laki 1 kwa mwaka,fedha hizo ni bajeti katika kipindi mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea pori hilo Mhifadhi Mwandamizi kutoka TAWA Mpanga-Kipengere Alfred Kipondamali alisema fedha hizo zilizotengwa zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kitalii katika maeneo ya kimani itakayogharimu shilingi 90 milioni sambamba na kuboresha maisha ya watumishi katika pori hilo.
Kipondamali ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa pori la Akiba Mpanga-Kipengere alisema ujenzi huo utahusisha ujenzi wa Campsite yenye thamani ya shilingi 120 milioni, ujenzi wa daraja lenye thamani ya shilingi 70 milioni litakalowezesha watalii kutoka maeneo ya Kimani kufika eneo la Ikovu na kuondoa adha ya ukosefu wa barabara ya uhakika ya kuingia hifadhini.
Alitaja vingine kuwa ni ujenzi wa geti la watalii lenye thamani ya sh 200 milioni, ujenzi wa nyumba ya watumishi yenye thamani ya sh 102 milioni sambamba na ujenzi wa barabara unaendelea kwa sasa wenye thamani ya sh 180 milioni unaofanywa na kampuni ya SUMA JKT utakaowezesha watalii kutoka eneo la Kimani lililopo barabara ya Iringa kwenda Mbeya hadi kufika kwenye maporomoko ya Kimani yaliyopo kwenye pori la akiba Mpanga-Kipengere.
Alisema uwekezaji huo uliofanywa na TAWA utasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka 7,000 ambao wanapokewa kwa mwaka kwa sasa hadi kufikia watalii laki moja kwa ndani na nje ya nchi.
Mhifadhi Mwandamizi Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Pori la Akiba la Mpanga-Kipengere Alfred Kipondamali akionyesha ramani ya Pori hilo na kuzungumza na waandishi wa habari walifika katika Ofisini kwake kwa ajili ya kupata maelezo juu ya Pori la Akiba Mpanga Kipengere linavyokusudia kuongeza watalii kutoka watalii 7,000 hadi kufika watalii laki Moja kwa Mwaka moja.(Picha Lilian Lucas)
“Ni kwamba awali watalii walikuwa wakifika na kulala kwenye mahema ambapo kwa sasa ujenzi huu utasadia kuwa na mahali pa kulala, kupumzika na kuongeza thamani ya utalii katika pori hili,”alisema Kipondamali.
Awali Kipondamali alisema pori hilo lilianzishwa mwaka 2002 likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 1,524 likiwa ndani ya mikoa ya Mbeya kwenye Wilaya ya Mbarali na Njombe kwenye Wilaya ya Wanging’ombe na Makete.
Alitaja malengo ya kuanzishwa pori hilo ni kutunza hifadhi ya vyanzo vya maji ambapo pori hilo linachangia zaidi ya asilimia 40 ya maji yanayoenda kwenye mabwawa makubwa ya kutengeneza umeme ya kidatu na Mtera sambamba na Bwawa na Mwalimu Nyerere.
“Kwa kifupi maji haya yana matumizi tofauti, baada ya kutoka hifadhini, huwa yanaenda kwa ajili ya shughuli za kilimo katika wilaya ya Mbarali, yanaingia mto Ruaha, mto ruaha yanaenda bwawa la Mtera ambapo yanazalisha umeme, yanaenda bwawa la kidatu na kwenda kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere,” alisema.
Pia, alitaja malengo mengine kuwa ni kutunza rasilimali za wanyama wa asili pamoja na kupanua wigo wa shughuli za utalii zilizopo katika nyanda za juu kusini ambapo alitoa wito kwa watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika pori hilo ikiwemo maporomoko saba makubwa ya maji, maua mbalimbali ya asili ambayo mengine hayapatikani popote duniani, mapango ya Chifu Mkwawa aliyojificha kwenye mapigano na wajerumani na safu za milima mikubwa ya mpanga na kipengere.
Naye, Kaimu Kamishna msaidizi mwandamizi wa Mahusiano kwa Umma TAWA Twaha Twaibu aliwashauri wazazi kuona umuhimu wa kuhamasika katika utalii kwa kuwahimiza watoto kuangalia televisheni ya Taifa kipindi cha wanyama.
"Tuwapeleke watoto wetu kwenye kuangalia vivutio vya utalii vilivyopo, isijefika mahali mtoto anakuwa mkubwa akiilizwa yule mnyama gani anatamka mnyama mwingine, ni aibu" alisema Twaibu.
Alisema hiyo itasaidia kukuza utalii na kuleta maana ya dira ya maliasili kuwa 'tumerithishwa tuwarishishe' na watoto wetu.
TAWA ina mapori ya akiba zaidi ya 20 ambayo
huyatumia katika kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo wanyama, misitu na safi
za milima zilizojaa maua.
No comments:
Post a Comment