Breaking News

Jul 27, 2021

RC SHIGELA ATOA TAHADHARI YA CORONA KWA WANANCHI MOROGORO


                   MKUU WA MKOA WA MOROGORO,MARTINE SHIGELA

RC SHIGELA ATOA TAHADHARI YA CORONA KWA WANANCHI MOROGORO

Na Lilian Lucas,Morogoro 

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka wananchi mkoani hapo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kuvaa barakoa, kutokusanyika sehemu moja bila sababu ya msingi, kunawa mikono kwa maji tiririka, na kufuata ushauri wa wataalamu unaotolewa na Wizara ya afya.

Shigela alitoa tahadhari hiyo kwenye kikao cha kutathimini cha nusu mwaka cha mkataba wa lishe na Bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa(ICHF) Manispaa ya Morogoro.

Alisema,mkoa wa Morogoro bado una changamoto ya ugonjwa wa Corona na maelekezo ya wataalamu yamekuwa yakielekeza vizuri namna ya kuchukua tahadhari hivyo kama viongozi lazima waendelee kuwaepusha na kuwakumbusha wananchi.

“Kama unaona kwamba kuna mkusanyiko na mimi sina ulazima wa kushiriki hakuna sababu ya kufanya hivyo, kama kuna umuhimu wa kwenda kanisani ama msikitini chukua tahadhari, 'social distance', uvaaji barakoa na kunawa maji tiririka lakini kama upo kwenye mazingira ambapo maji hayapo chukua santizer,”alisema.

Alisema na kama yote hayo yamefanyika na bado ukajiona una maambukizi ama dalili za Corona ni vyema kutosubiri bali ni kuwahi katika vituo vya kutolea huduma ili kupewa tiba mapema.

“Watu wengi wanakimbilia kwenye tiba kwa ugonjwa huu wa Corona, ama vituoni wakiwa wamechelewa ama wakiwa na hali mbaya ya kulazimika kuwekewa Oxygen na baadae kupelekea kupoteza maisha,”alisema.

Pia aliwataka wale watumiaji wa vyombo vya usafiri, waendaji sokoni, Standi, Misikitini na Makanisani, wale watoa huduma zenye mikusanyiko kujikinga kwa kuchukua tahadhari ya hali ya juu kwa kukaa umbali wa zaidi ya mita moja.

Baadhi ya wananchi waliozungumza juu ya tahadhari ya Corona inazoendelea kutolewa na serikali walisema bado wengi wao hawafuati maelekezo na wengine wamekuwa wakionyesha kudharau kutumia kinga kama barakoa.

Mkazi wa mtaa wa Kilombero Amina Said alisema “Kusema kweli serikali inajitahidi kutueleza namna ya kujikinga lakini wengi wetu si wasikivu wanaona kama hili jambo ni la watu fulani tumekuwa tukijisahau, labda niwaombe tu watanzania wenzangu tuendelee kufuata masharti na maelekezo yote,”. 

Said, alisema kama tahadhari itachukuliwa na kufuatwa na kila mmoja ni imani yake kuwa Ugonjwa huo wa Corona hautaendelea kushambulia watu.

Mganga mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kusirye Ukio aliulizwa kwa sasa hali ya Corona na idadi ya wagonjwa kimkoa alisema taarifa zote zinatolewa na wizara ya Afya na kama mkoa jukumu lao ni kuzipeleka wizarani.

 

No comments:

Post a Comment