Breaking News

Feb 18, 2021

TANESCO PWANI YAPONGEZWA KUBORESHA MIUNDOMBINU


MKUU WA MKOA WA PWANI,MHANDISI EVARIST NDIKILO(KATIKATI) AKISISIZA JAMBO WAKATI AKIPOTEMBELEA KITUO CHA KUPOZA UMEME MLANDIZI-KIBAHA PWANI.


TANESCO PWANI YAPONGEZWA KUBORESHA MIUNDOMBINU

NA VICTOR MASANGU, PWANI

SERIKALI Mkoani Pwani, imesema kwamba Kituo  cha kupoza umeme kilichopo Mlandizi, Wilayani Kibaha, ambacho kilipatwa na majanga ya kuungua na moto mwezi Machi mwaka jana,   hatimaye kimefanyiwa matengenezo  na  kinatarajia kuanza kufanya kazi rasmi  mwezi Machi 2021  ambapo kitatoa  huduma ya utoaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani   ikiwemo  Wilayani za Kibaha pamoja na  Bagamoyo.

 Hayo yalibainishwa  na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Injinia Evarist Ndikilo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja kwa ajili ya kutembelea na kujionea maendeleo na matengenezo mbalimbali katika kituo hicho ambapo ameupongeza uongozi wa  Shirika la umeme Tanesco Mkoa wa Pwani  kuweza kuboresha miundombinu ambayo ilikuwa imeharibika  hapo awali na kuwa kero  kubwa kwa wananchi hao kukosa umeme.

Ndikilo alifafanua kwamba, baada ya kutokea kwa janga la moto katika kituo hicho cha umeme Mlandizi, baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati hiyo ya umeme kutokana na kukatika mara kwa mara lakini kutokana na juhudi ambazo zimefanyika na Tanesco Mkoa wa Pwani kero hiyo sasa inakwenda kumalizika pindi ifikapo mwezi wa tatu mwaka huu.

“Kwa kweli mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Pwani nimefarijika sana na napenda kuchukua fursa hii kulipongeza sana tena sana Shirika la umeme Tanesco Mkoa wa Pwani kutokana na kuonyesha nia  ya kufanya yale yote ambayo tulikubaliana na kwa kweli kwa upande wangu nipende kusema kwamba nimeridhishwa na ukarabati na ujenzi ambao umefanyika hii ni dalili nzuri katika Mkoa wetu wa Pwani kuwa na nishati ya Uhakika.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani, alisema kwamba, kwa sasa  mahitaji ya umeme Katika Mkoa  ni yanayohitajika ni megawatt zipatazo 117.8 na kwamba  kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa kituo hicho ni moja ya kuleta maendeleo makubwa katika kukuza uchumi pamoja na kuwavutia wawekezaji mbali wa ndani na nje ya nchi.

Kadhalika, alizitaka mamlaka nyingine  ikiwemo Dawasa pamoja na TANRODS kuhakikisha kwamba wanaweka mipango endelevu ya kudumisha huduma zao kwa wananchi ikiwemo kurekebisha miundombinu mbalimbali ya barabara ili iweze kupitika kwa urahisi kuingia kwenye viwanda ambavyo vipo katika Mkoa wa Pwani.

“Tanesco leo kwa kweli nimetembelea kituo hiki cha kupozea umeme wamenifurahisha sana kwa kuwa nimejionea mimi mwenyewe kwa jinsi walivyofunga mitambo na laini mbalimbali ambazo zinatumika katika kuwasambazia umeme wateja mbalimbali wa Wilaya ya Kibaha, pamoja na Bagamoyo pamoja na katika maeneo ya viwanda na hi ni hatua kubwa kwa hivyo na taasisi zingine kama Dawawa na Tanrods na wao waige mfano huu wasifanya kazi mezani ila wafanye kwa vitendo kama Tanesco.

Ndikilo,pamoja na kulipongeza Shirika hilo la Tanesco Mkoa wa Pwani, lakini pia amelitaka lifanye jitihada za makusudi katika kupelekeka umeme wa uhakika katika Wilaya ya Mkuranga ambayo nao inauwekezaji mkubwa wa viwanda na kujenga kituo maalumu cha kupozea umeme ambacho kitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuliko kutegemea kwa kiasi kikubwa umeme kutoka katika kituo cha Mbagala kilichopo Jijini Dar es Salaam. 

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la umeme Tanesco, Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mahawa Mkaka, amebainisha kwamba kituo hicho mwaka jana kiliweza kuungua na kusababisha hasara kubwa na kusababisha changamoto kubwa ya baadhi ya maeneo   kukatika katika kwa umeme mara kwa mara na kwamba kituo hicho kitakuwa  mkombozi mkubwa kwa wananchi kupata umeme wa uhakika.

Naye, Mkuu wa kituo hicho cha kupozea umeme cha Mlandizi,Baraka Zonga kituo hicho cha kupoozea umeme kina transfoma kubwa nne amabzo zitakuwa na uwezo wa kusambaza umeme katika laini saba katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika mitambo ya  maji ya Ruvu juu pamoja na ile ya Ruvu chini sambamba na maeneo mengine ya viwanda na bandari kavu ya Kwala.

Mkoa wa Pwani kwa sasa imetajwa kuwa kinara katika uwekezaji wa viwanda hivyo kuboresha kwa miundombinu ya umeme na kuanza  kufanya kazi  tena kwa kituo hicho cha kupoozea umeme Mlandizi kitaweza kuwa ni Mkombozi mkubwa kwa wananchi pamoja na wawekezaji wa viwanda kupata  umeme wa uhakika.


No comments:

Post a Comment