BONDE LA WAMI RUVU WAJA NA MPANGO WA KUDHIBITI UHARIBIFU WA VYANZO VYA MAJI
Hamida Shariff, Morogoro
KUPUNGUA
kwa maji katika vyanzo vya maji vya Bonde la Wami Ruvu, kunasababishwa na
shughuli mbalimbali za kijamii kikiwemo Kilimo, ufungaji na uchimbaji madini.
Hayo yalisemwa jana, na
kaimu Katibu tawala mkoa wa Morogoro anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi
Ezron Kilamhama wakati akifungua kongamano la wadau wa maji Bonde la Wami Ruvu
lililolenga kujadili mpango wa namna ya kudhibiti uharibifu wa mazingira kwenye
vyanzo vya maji katika bonde hilo.
Mhandisi Kilamhama, alisema
kuwa kupungua kwa kina cha maji kwenye vyanzo vya maji vya Bonde la Wami Ruvu
kunaathiri shughuli za uchumi kwa kuwa rasilimali ya maji inategemewa katika
shughuli za Kilimo, ufugaji, viwanda, madini na matumizi ya majumbani hivyo
lazima iwekwe mipango na mikakati ya kusimamia vyanzo vya maji.
Alisema kuwa, kwa kutambua
umuhimu wa rasilimali za maji, Wizara iliajiri mtaalamu mshauri wa kuandaa
mpango shirikishi wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika Bonde
la Wami Ruvu.
Aidha, alisema kuwa mpango
huo unaainisha mahitaji ya wadau mbalimbali wa sekta ya maji kwa kuzingatia
wakati uliopo na wakati ujao.
Mhandisi Kilamhama, alisema
kuwa Wizara iliajiri mtaalamu mshauri
ambaye anaandaa mpango mkakati wa tathiminj ya athari za mazingira na jamii.
Akieleza athari walizobaini katika tathimini hiyo, muikolojia na mtaalamu wa mazingira, Asukile Kajuni alisema kuwa, athari walizobaini zinatokana na shughuli za kibinadamu, hata hivyo kupitia mipango mikakati athari hizo zinaweza kudhibitiwa.
Alisema kuwa, kama
hakutakuwa na mipango madhubuti, kina cha maji katika Bonge la Wami Ruvu
kitaendelea kupungua na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi.
Miongoni mwa wadau
walioshiriki kongamano hilo, ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa,
Asajile Mwambambale ambaye alisema suala la ushirikishwaji katika utekelezaji
wa mipango hiyo itasaidia kufikia lengo la kutunza vyanzo vya maji.
Mwambambale, alisema kuwa, Halmashauri
ya Wilaya ya Kilosa ni moja ya maeneo yenye shughuli za ufungaji, Kilimo na
uchimbaji hivyo mpango huo utasaidia kusimamia shughuli hizo ili kudhibiti
uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji unaofanywa kupitia sekta hizo.
Mwenyekiti wa bodi ya maji,
Bonde la Wami Ruvu,Hamza Sadiki alisema kuwa mpango huo ndio suluhisho la
uharibifu wa vyanzo vya maji katika Bonde la Wami Ruvu.
No comments:
Post a Comment