Breaking News

Aug 5, 2022

Pinda ashtushwa na udumavu kwa watanzania kwa ‘kukosa lishe’


WAZIRI MKUU MSTAAFU,MIZENGO PINDA

Pinda ashtushwa na udumavu kwa watanzania kwa ‘kukosa lishe’

Lilian Lucas,Morogoro

WAZIRI mkuu mstaafu awamu ya nne, Mizengo Pinda amesema suala la utapiamlo linatakiwa kuendelea kupigiwa kelele kwani bado ni kubwa kwa nchi ya Tanzania na hiyo inapelekea  udumavu kwa asilimia 31 kwa watu wake.

Alisema hayo wakati wa ufunguzi  wa maonyesho ya nanenane kanda ya mashariki yanayoshirikisha mikoa ya Pwani, Dar es salaam, Tanga na Morogoro  yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere.

Alisema suala la lishe bora ni vyema likapigiwa kelele na kuacha kubebeshwa lawama serikali kutokana na watoto wanaozaliwa na kwamba wataalamu wamekuwa wakieleza kuwa akinamama wajawazito wengi wamekuwa na upungufu wa damu na kuelekea kujifungua kwa matatizo na hiyo ni kutokana na kula vyakula bila kujali lishe bora.

“Mimi natoka Katavi tunatamba kwa kulima mahindi lakini ugali wa mahindi niliozoea ni kwamba ukobolewa, ulowekwe kwenye maji wiki moja halafu uanikwe kidogo na kupelekwa kusangwa mashine eti kupata ugali mzuri wa kunukia hii si hoja,”alisema na kuongeza,

“Kumekuwa na mazoea kuwa wanaokula dona ni wafungwa pekee na hii si sawa pale watu wengi wanakula wanga (starch) ndani yake hakuna kitu sasa tuna mtihani mkubwa wa kusemea lishe.”

Aidha, alisema pamoja na mikoa  ya Rukwa na Katavi kuongoza katika kulima zao la mahindi lakini mkoa hiyo ni moja ya inayoongoza katikasuala zima la utapiamlo.

Alisema wataalamu wamekuwa wakieleza kuwa ili kokomesha suala la utapiamlo ni lazima watu watumie mbogamboga kama chakula muhimu na kwamba ulimwengu unakili kuwa mboga zenye asili ya Afrika zimekuwa zikiongoza kwa lishe.

“Nataka tutoke hapa kwenda kulima bustani za mboga na sio kulima kwa ajili kulima kula ilikuweza kupata afya bora, hivyo nanenane kwangu tutumie kujifunza kilimo hicho,”alisema.

Pia waziri mkuu huyo mstaafu aliwataka wananchi kutumia ufugaji bora huku akieleza kufurahishwa na ufugaji bora hasa wa Samaki  kwa kutumia njia za kisasa.

Alisema sekta ya kilimo bado ni muhimili kwa nchi hivyo kilimo kikiteteleka ni kama mtu akiteteleka na mgongo wake hivyo ni muhimu  katika kuleta maendeleo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema wizara katikakuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukijitokeza imeanzisha  mfumo wa mazao ya Uvuvi, mifugo na mazao mengine (MIMIS) utakao wawezesha wadau wa mifugo wa zao ya uvuvi kufanya shughuli zao kwa haraka kama kuomba kibali na chochote kwa urahisi.

Ndani alisema pia Wizara imekuwa na teknolojia  mpya itakayowezesha wadau kupima maziwa ubora wake kwa urahisi zaidi na hiyo iko katika mfumo.

Aidha alisema wizara inaendelea kufanya mabadiliko katika mifumo mbalimbali ya kuoa urasimu na kuwataka wananchi kuondoka kwenye mifumo ya zamani, wizara inaendelea kuhamasisha wafugaji na wananchi kwa ujumla kuhusiana na chanjo mbalimbali za mifugo na sasa aina saba za chanjo zinazalishwa na kiwanda cha serikali.

No comments:

Post a Comment