Breaking News

Aug 31, 2021

TUGHE MKOA WA PWANI YAPATA VIONGOZI WAPYA


Mwenyekiti  wa  Chama cha wafanyakazi wa serikali na afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Pwani  Catheline Katele akitoa neno la shukrani kwa wajumbe mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ambapo ameweza kuibuka mshindi kwa kupata kura 48 dhidi ya 51 ambazo zimepigwa


TUGHE MKOA WA PWANI YAPATA VIONGOZI WAPYA

NA VICTOR MASANGU, PWANI

CHAMA  cha wafanyakazi wa serikali na afya Tanzania (TUGHE), Mkoa wa Pwani umefanya uchaguzi wake mkuu na kufanikiwa kupata safu ya viongozi wapya katika nafasi mbalimbali huku Mwenyekiti wake akiibuka kuwa ni Catheline Katele ambaye ataongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani uliweza kuhudhuriwa na wajumbe kutoka katika Wilaya zote saba uliweza pia  kusimamia na afisa kazi wa Mkoa wa Pwani ambapo mwenyekiti huyo aliweza kuibuka na ushindi baada ya kupata kura 48  dhidi ya 51 ambazo  zilizopigwa na mpinzani wake  Dr. Alphonce Moyo akipata kura tatu.

Mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo Mwenyekiti  huyo wa mpya wa  Chama cha wafanyakazi wa serikali na afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Pwani Catherine Katele aliwashukuru wajumbe wote ambao wamemchagua na kuahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kila Nyanja ili kuwaletea maendeleo.

Pia Mwenyekiti huyo ameahidi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi ikiwemo kupatiwa stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria  na taratibu ikiwemo kupandishwa madaraja pamoja na mishahara.

“Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa siku ya leo nimeweza kupata fursa hii ya kuchaguliwa tena katika kipindi cha miaka mitano lakini kitu kikubwa nitahakikisha kwa upande wangu ninashirikiana na viongozi wenzangu katika kuweka mipango mizuri ambayo itawasaidia wafanyakazi kuweza kupata stahiki ikiwemo mupandishwa madaraja pamoja na mishahara” alisema

Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo mkuu kutoka Wilaya mbali mbali za Mkoa wa Pwani wakiwa wametulia kusikiliza maelekezo ambayo yalikuwa yanatolewa na msimamizi wa uchaguzi ambaye hayupo pichani.

Aidha, Katele alisema kwamba anatambua wafanyakazi wa Mkoa wa Pwani baadhi yao bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo jambo hilo kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita ambayo inaongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan linafanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali lengo ikiwa ni kuwapa wafanyakazi stahiki zao kwa wakati.

Pia, katika hatua nyingine aliongeza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa weledi na msingi iliyowekwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zote na kubainisha kuwa  atakuwa mzalendo katika kuwatumikia wafanyakazi wote bila ya upendeleo na ubaguzi  wowote kwa maslahi ya Taifa.

Naye mmoja wa  mjumbe ambaye amechaguliwa kwa kura 32  katika nafasi ya   mkutano mkuu ngazi ya Taifa Dkt. Michael Benedict amebainisha mipango yake ambayo ataipambania kwa hali na mali kwa lengo la kuweza kushirikiana na viongozi wenzake kwa ajili ya  kuleta mbadailiko chanya ya kimaendeleo pasipo ubaguzi wowote.

Kwa upande wake  aliyeshinda katika nafasi ya mwakilishi wa vijana Mkoa wa Pwani Violeth Mahundi ambaye aliibuka kwa kupata kura 42  kati ya 51 zilizopigwa na kuahidi  kuweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia vijana waweze kutambua wajibu wao, haki na sheria za kazi na kuwaasa kachana na tabia ya utumiaji wa madawa ya kulevya.

uchaguzi  huo, umesimamiwa na afisa kazi Mkoa wa Pwani Razina Tunga ambapo   nafasi mbali mbali ziliweza kuchagaliwa zikiwemo za nafasi ya Mwenyekiti, nafasi za wajumbe wane  wa mkutano mkuu Taifa,nafasi wajumbe  watatu wa kamati ya utendaji ngazi ya Mkoa,mjumbe wa baraza kuu,mwakilishi wa walemavu,  mwakilishi wa  vijana pamoja na nafasi mbali mbali.

No comments:

Post a Comment